Nafasi Ya Matangazo

August 15, 2012

JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
 
WIZARA YA FEDHA
HOTUBA YA WAZIRI WA FEDHA
MHE. DKT. WILLIAM AUGUSTAO MGIMWA (MB) AKIWASILISHA BUNGENI MAKADIRIO YA MAPATO NA MATUMIZI YA WIZARA YA FEDHA KWA MWAKA 2012/13


UTANGULIZI
Mheshimiwa Spika, kufuatia taarifa iliyowasilishwa hapa Bungeni na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Fedha na Uchumi, naomba kutoa hoja kwamba Bunge lako Tukufu likubali kupokea, kujadili na kupitisha Makadirio ya Mapato, Matumizi ya Kawaida na ya Maendeleo ya Wizara ya Fedha kwa mwaka wa fedha 2012/13.

Mheshimiwa Spika,  awali ya yote napenda kutumia fursa hii kutoa pongezi zangu za dhati kwako pamoja na Naibu Spika Mheshimiwa Job Yustino Ndugai, Mbunge wa Kongwa, Waheshimiwa Wenyeviti Jenista Joakim Mhagama (Mbunge wa Peramiho), Sylivester Massele Mabumba (Mbunge wa Dole) na Mussa Azzan Zungu (Mbunge wa Ilala), kwa kuongoza vema majadiliano ya Bunge la Bajeti.

Mheshimiwa Spika, naomba nitumie nafasi hii kuishukuru kwa namna ya pekee Kamati ya Fedha na Uchumi chini ya Mwenyekiti wake Mheshimiwa Mtemi Andrew John Chenge, Mbunge wa Jimbo la Bariadi Mashariki kwa maoni, ushauri na mapendekezo waliyoyatoa kwa Wizara wakati wa kuchambua mapendekezo ya Bajeti ya Wizara ya Fedha. Wizara imezingatia ushauri na mapendekezo ya Kamati katika kukamilisha uandaaji wa hotuba hii.

Mheshimiwa Spika, napenda pia kutumia fursa hii kuwashukuru Naibu Mawaziri, Mheshimiwa Janet Z. Mbene (Mb), na Mheshimiwa Saada M. Salum (Mb) pamoja na Katibu Mkuu Ndugu Ramadhan M. Khijjah na Manaibu wake Ndugu Laston T. Msongole, Dkt. Servacius B. Likwelile na Ndugu Elizabeth J. Nyambibo kwa kazi kubwa wanayoifanya ya kusimamia utekelezaji wa majukumu ya Wizara. Aidha, nawashukuru Wakuu wa Idara na Vitengo, Wakuu wa Taasisi na Wakala wa Serikali, chini ya Wizara na wafanyakazi wote wa Wizara ya Fedha kwa kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi .

Mheshimiwa Spika, naomba sasa, uniruhusu nisome maelezo haya kwa muhtasari na hotuba nzima iingie kwenye Hansard.


MAPITIO YA UTEKELEZAJI WA MPANGO NA BAJETI YA WIZARA KWA MWAKA 2011/12

Mheshimiwa Spika, Wizara imeendelea kutekeleza majukumu yake kupitia mafungu manne ya kibajeti. Mafungu hayo ni Fungu 50 - Wizara ya Fedha; Fungu 21 – HAZINA; Fungu 22 - Deni la Taifa; Fungu 23 - Ofisi ya Mhasibu Mkuu wa Serikali na - Fungu 45 Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi.
                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                  
Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2011/12, Wizara kwa kuzingatia jukumu lake la msingi la kukusanya mapato na kusimamia  matumizi ya fedha za umma, ilijikita katika kutekeleza yafuatayo:
Kubuni na kusimamia utekelezaji wa Sera za Uchumi Jumla;
Kusimamia na kuratibu shughuli  za Taasisi na mashirika ya umma;
Kukusanya mapato ya ndani yasiyopungua shilingi bilioni 6,435.28. Kati ya hizo shilingi bilioni 6,228.80 ni mapato ya kodi na shilingi bilioni 206.48 ni mapato yasiyo ya kodi;
Kujenga uwezo wa uandaaji na usimamizi wa Bajeti ya Muda wa Kati pamoja na utoaji wa taarifa za utekelezaji kwa wakati;
Kuendelea na ukaguzi wa ndani na kuimarisha Idara ya Mkaguzi wa Ndani Mkuu wa Serikali;
Kusimamia utekelezaji wa bajeti ya serikali na uratibu wa utekelezaji wa MKUKUTA;
Kusimamia deni la taifa;
Kusimamia na kuhakiki malipo ya mishahara ya watumishi wa Serikali na Taasisi zake;
Kuendeleza kada za Uhasibu, Ukaguzi wa Ndani, Ununuzi na Ugavi, Uchumi, Uhakiki Mali, Mipango, Usimamizi wa Fedha, Watakwimu na Wataalamu wa Kompyuta;
Kuendelea kuhuisha Daftari la Mali ya Serikali;
Kuendelea na ukaguzi wa miradi ya maendeleo na kusimamia utekelezaji wa miradi inayofadhiliwa na Serikali ya Marekani kupitia Shirika la Millennium Challenge Corporation (MCC);
Kuendelea kuboresha utoaji wa huduma za mafao ya wastaafu na mirathi;
Kuimarisha Mtandao wa Malipo - IFMS katika ngazi zote za Serikali, na kusambaza  matumizi ya mfumo wa malipo kwa njia ya elektroniki  katika HAZINA ndogo na Sekretarieti za Mikoa;
Kutoa mafunzo ya kuandaa hesabu za serikali katika viwango vya kimataifa;
Kuhamasisha  ushiriki wa Sekta binafsi katika utekelezaji wa miradi ya ubia; na
Kutoa mikopo kwa asasi ndogo za fedha kupitia Mradi wa Mikopo kwa Wajasiriamali Wadogo (Small Enterprise Loans Facility Project - SELF) na kuongeza kasi ya ukusanyaji wa madeni ya mikopo hiyo.

UTEKELEZAJI WA MAJUKUMU KWA MWAKA 2011/12 NA MALENGO YA MWAKA 2012/13
                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                       
Ukusanyaji wa Mapato kwa Mwaka 2011/12

Mheshimiwa Spika, kuanzia Julai 2011 hadi Juni, 2012 mapato ya kodi yaliyokusanywa na Mamlaka ya Mapato Tanzania yalifikia shilingi bilioni 6,511.2, sawa na asilimia 104.5 ya lengo la mwaka la kukusanya shilingi bilioni 6,228.8 . Aidha, Wizara ilikusanya mapato yasiyo ya kodi kiasi cha shilingi bilioni 214.62 sawa na asilimia 103.9 ya lengo la mwaka la kukusanya shilingi bilioni 206.48. Kufikiwa kwa malengo ya makusanyo ya mapato ya kodi kumetokana na kuboresha usimamizi wa ukusanyaji wa mapato.

Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2012/13, ukusanyaji wa mapato utaendelea kuimarika kwa kuchukua hatua za kisera na kiutawala kwa maeneo ya mapato ya kodi na yasiyo ya kodi. Kwa kuzingatia hatua hizo, mapato ya kodi kwa mwaka 2012/13 yatakayokusanywa na Mamlaka ya Mapato Tanzania yamepangwa kufikia shilingi bilioni 8,070.09. Aidha, mapato yasiyokuwa ya kodi yamepangwa kufikia shilingi bilioni 124.42 kwa kipindi hicho.

Misaada na Mikopo
Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2011/12, Wizara ilipanga kukusanya mapato kutokana na misaada na mikopo kutoka nje ya nchi yenye thamani ya shilingi bilioni 3,923.55. Kati ya fedha hizo, shilingi bilioni 869.41 ni misaada na mikopo ya kibajeti na shilingi bilioni 2,366.14 ni misaada na mikopo ya miradi ya maendeleo na shilingi bilioni 688 ni misaada na mikopo ya mifuko ya kisekta. Hadi kufikia mwishoni mwa Juni, 2012 misaada na mikopo iliyopokelewa ilikuwa shilingi bilioni 2,488.3 sawa na asilimia 63 ya makadirio ya mwaka. Kati ya fedha hizo, shilingi bilioni 916 sawa na asilimia 105 ya makadirio ilikuwa misaada na mikopo ya kibajeti na shilingi bilioni 1,571.9 sawa na asilimia 51 ya makadirio ilikuwa misaada na mikopo ya miradi ya maendeleo na mifuko ya kisekta.

Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2012/13, Wizara imelenga kukusanya mapato ya shilingi bilioni 3,229.0 kutokana na misaada na mikopo kutoka nje. Kati ya fedha hizo, shilingi bilioni 842.48 ni misaada na mikopo ya kibajeti, shilingi bilioni 1,971.40 ni misaada na mikopo ya miradi ya maendeleo ikijumuisha shilingi bilioni 72.3 marejesho ya fedha ya rada, na shilingi bilioni 415.14 ni misaada na mikopo ya mifuko ya kisekta.

Usimamizi wa Deni la Taifa
Mheshimiwa Spika, Wizara ya Fedha imeendelea kusimamia deni la taifa kwa kuzingatia Mkakati wa Kusimamia Deni la Taifa wa mwaka 2002 pamoja na Sheria ya Mikopo, Dhamana na Misaada Na. 30 ya mwaka 1974 pamoja na marekebisho yake ya mwaka 2004. Hadi mwishoni mwa Juni 2012, Deni la Taifa (debt stock) lilikuwa shilingi bilioni 20,865.0 ikilinganishwa na deni la shilingi bilioni 18,617.0 Juni 2011 ikiwa ni sawa na ongezeko la asilimia 10.7. Kati ya hizo, shilingi bilioni 15,927.1 zilikuwa ni deni la nje na shilingi bilioni 4,937.9 ni deni la ndani. Kati ya kiasi cha deni la nje, shilingi bilioni 12,644.6 zilikuwa ni deni la umma na kiasi kilichobaki cha shilingi bilioni 3,282.5 ni deni la sekta binafsi. Aidha, hadi kufikia Juni 2012, deni la ndani la Serikali lilifikia shilingi bilioni 4,937.9 ikilinganishwa na shilingi bilioni 4,729.0 mwezi Juni, 2011, sawa na ongezeko la asilimia 4.2.

Mheshimiwa Spika, Sera za Bajeti na Fedha (Fiscal & Monetary policies) zinajumuisha mikopo ya ndani na nje. Kuongezeka kwa Deni la Taifa kumetokana na mikopo mipya ya ndani na nje inayokopwa ili kuziba nakisi ya bajeti ya maendeleo. Hadi kufikia Juni 2012, malimbikizo ya deni kwa nchi ambazo bado hazijatoa misamaha yalifikia Dola za Marekani milioni 907.24. Nchi hizo ni Brazil ambayo iko kwenye kundi la Klabu ya Paris ambayo malimbikizo ya deni kwa nchi hiyo ni Dola za Marekani milioni 239.6. Nchi nyingine ambazo zipo kwenye kundi lisilo la Klabu ya Paris ni Iran (Dola za Kimarekani milioni 372.03), Iraq (Dola za Kimarekani milioni 290.1) na Angola (Dola za Kimarekani milioni 5.51). Majadiliano ya msamaha wa madeni baina ya Serikali na nchi hizo yanaendelea na yamefikia katika hatua nzuri ya kufikia makubaliano.

Mheshimiwa Spika, malipo ya deni la Taifa hufanyika kupitia Fungu 22 - Deni la Taifa. Katika kipindi cha kuanzia Julai, 2011 hadi Juni, 2012, malipo ya deni la ndani yalikuwa shilingi bilioni 1,671.71 na malipo ya deni la nje yalikuwa shilingi bilioni 125.15. Aidha, madai na madeni mengine hulipwa kupitia mafungu ya wizara husika.

Mheshimiwa Spika, ili kuongeza ufanisi katika kuratibu na kusimamia Deni la Taifa katika mwaka wa fedha 2012/13, Wizara imepanga kufanya marekebisho katika Muundo wake kwa kuanzisha Idara kamili ya usimamizi wa Deni la Taifa ambayo pia itakuwa na wataalam wenye weledi katika masuala ya mikopo ya kibiashara.
Uandaaji, Usimamizi na Ufuatiliaji wa Utekelezaji wa Bajeti ya Serikali kwa mwaka 2011/12

Mheshimiwa Spika, katika kutekeleza majukumu yake, Wizara  iliandaa, kusimamia  na kufuatilia utekelezaji wa Bajeti ya Serikali. Kazi zilizofanyika ni pamoja na kuandaa Mwongozo wa Mpango na Bajeti  kwa mwaka wa fedha 2012/13 ambao unatekeleza Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano 2011/12 - 2015/16. Mwongozo huo ulisambazwa kwa Wizara, Idara zinazojitegemea, Taasisi na Wakala za Serikali, Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa na umetumika katika kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa mwaka 2012/13.

Mheshimiwa Spika, ili kuboresha malengo, matokeo na utoaji wa taarifa za utekelezaji wa bajeti ya Serikali, Wizara imeandaa taarifa mbalimbali zikiwemo: Vitabu vya bajeti; Taarifa ya utekelezaji wa bajeti ya Serikali kwa mwaka 2011/12; Taarifa ya Uchambuzi wa Bajeti ya Serikali katika Kipindi cha Muda wa Kati (Budget Background and Medium Term Expenditure Framework – 2011/12 - 2012/13); Taarifa za madeni; Taarifa za mfumuko wa bei; Taarifa ya Hali ya Uchumi; Taarifa za kifedha kupitia Benki Kuu; Kitabu cha bajeti ya Serikali kwa lugha rahisi na kadhalika.

Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2012/13, Wizara inakusudia kuendelea kujenga uwezo kwa Wizara, Idara zinazojitegemea, Mikoa na Serikali za Mitaa kwa ajili ya kuandaa mipango na bajeti; kuandaa Mwongozo wa Mpango na Bajeti; kufuatilia matumizi ya fedha za Serikali; Kuandaa maelezo ya bajeti na kitabu cha bajeti ya Serikali kwa lugha rahisi. (Budget Background and Citizen Budget); na kuendelea kuboresha uandaaji wa bajeti.

Usimamizi wa Fedha za Umma.

Mheshimiwa Spika, Wizara  imeendelea kutekeleza Programu ya Maboresho ya Usimamizi wa Fedha za Umma. Katika mwaka wa fedha 2011/12, Wizara ilikamilisha utekelezaji wa awamu ya tatu ya programu hii ambapo mafanikio yaliyopatikana ni pamoja na: kuimarisha mfumo wa malipo kwa njia ya elektroniki  katika Wizara na Idara  zinazofanya malipo kupitia Ofisi Kuu ya Malipo Hazina; kutoa mafunzo ya “Cash Management” na malipo kwa njia ya elektroniki  kwa Wahasibu 304 kutoka Sekretarieti za Mikoa, HAZINA Ndogo, TAMISEMI, Ofisi ya Bunge na Tume ya Ushirika na Masoko; pamoja na kutoa mafunzo na kuandaa  Mwongozo wa Kihasibu wa kutumia viwango vya kimataifa vya kuandaa hesabu (IPSAS –Accrual) kwa Wahasibu wa Wizara, Idara, Mikoa na Balozi pamoja na Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC).
Mheshimiwa Spika, Wizara imeendelea kusimamia uendeshaji  wa mtandao wa malipo wa Serikali (Integrated Financial Management System – IFMS) kwa  kuziwezesha Wizara, Idara za Serikali na Mikoa kutumia mtandao  huo kwa ufanisi. Aidha, maboresho  ya mfumo   wa kihasibu wa ‘Epicor’ kutoka toleo namba 7.3.5  kwenda toleo namba 9.05 yamefanyika. Toleo hilo limeanza kutumika mwaka huu wa fedha wa 2012/13.

Mheshimiwa Spika, katika juhudi za kuboresha usimamizi na udhibiti wa matumizi ya fedha na mali ya Serikali, Wizara imeendelea kuwajengea uwezo wa kiutendaji Watumishi wa Kada za Uhasibu, Ununuzi na Ugavi, Ukaguzi wa Ndani na Mifumo ya Kompyuta. Kwa mwaka wa fedha 2011/12 Wizara imedhamini mafunzo ya muda mrefu kwa watumishi 263 wa kada hizo kutoka Wizara,  Idara za Serikali, Sekretarieti za Mikoa na Serikali za Mitaa katika vyuo mbalimbali nchini.

Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2012/13, Wizara inakusudia  kufanya yafuatayo: kudhamini watumishi wa Serikali katika vyuo mbalimbali vya Uhasibu na Kompyuta; kusimamia na kuimarisha uendeshaji na uunganishaji wa mtandao wa malipo wa Serikali; kutekeleza hatua za kuingia kwenye utaratibu wa kuandaa hesabu za Serikali kwa viwango vya kimataifa vya uhasibu; kuanza kutumia mfumo wa malipo wa elektroniki katika HAZINA ndogo na Mikoa yote; kuendelea kutoa miongozo ya kusimamia na kudhibiti mapato na matumizi ya Serikali; kusimamia mfuko wa mikopo kwa watumishi wa umma; kutengeneza VISA Stickers, kufunga mitambo ya kutolea VISA Stickers na kurekebisha mfumo wa kutolea VISA  kwenye Balozi zetu ili kudhibiti na kuongeza mapato ya Serikali; na kuimarisha usimamizi na utoaji wa taarifa mbalimbali za fedha.

Ukaguzi wa Ndani
Mheshimiwa Spika, ili kuimarisha uwazi na uwajibikaji wa matumizi ya rasilimali za umma, Wizara imeendelea kuimarisha Idara ya Mkaguzi wa Ndani Mkuu wa Serikali.  Kwa mwaka wa fedha 2011/12, Wizara imefanya yafuatayo: kuandaa Mpango Mkakati wa Ukaguzi wa Ndani; kutayarisha mwongozo wa kazi ya Ukaguzi wa Ndani na kutoa mafunzo ya mwongozo huo kwa wakaguzi wa ndani 500 kutoka Serikali Kuu na Serikali za Mitaa.  Aidha, katika juhudi za kuwajengea uwezo wakaguzi wa ndani, Wizara imeendelea kudhamini mafunzo ya muda mfupi katika kozi za kitaaluma za ukaguzi wa ndani, ukaguzi wa kiuchunguzi na mafunzo yaliyolenga maeneo hatarishi. Vile vile, mafunzo yalitolewa kwa kamati za ukaguzi za mamlaka za Serikali za Mitaa katika mikoa ya Dar es Salaam na Morogoro.

Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2012/13, Wizara kupitia Idara ya Mkaguzi wa Ndani Mkuu wa Serikali inakusudia kutekeleza yafuatayo: kukamilisha kanuni za maadili ya wakaguzi wa ndani Serikalini; kukamilisha mkataba wa makubaliano kati ya wakaguzi wa ndani na wateja wake; kuandaa mwongozo wa utekelezaji wa usimamizi wa vihatarishi (Guideline on Implementation of Institutional Risk Management Framework); kuhuisha mwongozo wa ukaguzi wa ndani wa Serikali kuu na Serikali za mitaa uendane na viwango vya kimataifa; kuandaa mpango mkakati wa Teknolojia ya Mifumo ya Fedha; kufuatilia utekelezaji wa mapendekezo ya taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali; kufanya ukaguzi wa miradi ya maendeleo na kutoa ushauri wa kitaalamu kwa watekelezaji wa miradi hiyo; kuandaa mwongozo wa uhakiki wa ubora wa ukaguzi wa ndani; na kuandaa mwongozo wa kamati za ukaguzi.

Ukaguzi wa Hesabu za Serikali
Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2011/12 Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali ilifanikiwa kutekeleza malengo yaliyopangwa. Ofisi iliweza kupanua wigo wa ukaguzi katika ngazi ya Halmashauri na kufika hadi vijijini kuhakiki utekelezaji wa miradi na matumizi ya fedha zinazotolewa kuendana na  Sera ya Ugatuaji wa Madaraka kwa Serikali za Mitaa (D-by-D). Aidha,  Ofisi iliweza kutoa ripoti tano za ukaguzi wa thamani ya fedha. Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali imeendelea kuimarisha kitengo cha ukaguzi wa Kiutambuzi (Forensic Audit) kwa kuwajengea uwezo wakaguzi wa kitengo hicho kwa kuwaambatisha kwenye ofisi za ukaguzi za nchi za nje zinazofanya vizuri katika eneo hilo. Vile vile, Ofisi imeweza kukamilisha ukaguzi kwa kutumia mifumo ya kompyuta (System Audit)  katika kaguzi zote.  Kadhalika, muundo mpya wa ofisi umeanza kutekelezwa kwa awamu ili kukidhi mahitaji ya Sheria ya Ukaguzi wa Umma Na.11 ya mwaka 2008. Ujenzi wa ofisi katika mikoa ya Kilimanjaro na Shinyanga pia umekamilika na ujenzi wa ofisi za Mikoa ya Dodoma na Rukwa umeanza. 

Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2012/13 ofisi itakuwa inatekeleza kwa mwaka wa pili Mpango Mkakati wa mwaka 2011/12 hadi  2015/16. Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi imelenga kutekeleza yafuatayo: kukagua mafungu 49 ya Wizara na Idara za Serikali, hesabu za Mikoa 21 ya Tanzania Bara, Hesabu za Halmashauri 134 za Miji, Wilaya, Manispaa na Majiji, Mashirika ya Umma 170, Balozi zote  zilizoko nje ya nchi na Wakala 33 za Serikali; kushiriki kikamilifu katika jukumu jipya la kukagua taasisi za Umoja wa Mataifa ambapo Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi imechaguliwa kuwakilisha Bara la Afrika katika Bodi ya Ukaguzi ya Umoja wa Mataifa (UN Board of Auditors). Aidha, Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi itaendelea na ujenzi wa majengo katika mikoa ya Dodoma na Rukwa pamoja na  kuanza ujenzi katika mikoa ya Mara na Iringa na kuanza ujenzi wa kituo cha mafunzo cha Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi (NAO training centre) katika eneo la Gezaulole – Kigamboni.

Usimamizi wa Mali ya Serikali
Mheshimiwa Spika,  katika mwaka 2011/12, Wizara imehakiki utunzaji wa mali ya Serikali na kutoa ushauri. Katika kulitekeleza hilo, uthamini wa mali umefanyika katika Wizara 20, Idara zinazojitegemea 12 na Mikoa minne na Mwongozo wa Usimamizi wa Mali ya Serikali ulitayarishwa. Aidha, wizara imehakiki mali katika bohari za Serikali 350 ambapo ushauri na taarifa zake zimetolewa kwa Maafisa Masuuli husika; kuondosha mali chakavu Serikalini kwa mujibu wa Sheria na Kanuni za Fedha ambapo jumla ya magari 145, Pikipiki sita, Mitambo 74 na vifaa mbalimbali vilihusika. Katika zoezi hilo, jumla ya shilingi bilioni 1.73 zilipatikana.


Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2012/13, Wizara itaendelea na kazi ya kuingiza kwenye Daftari mali ya Serikali iliyokwisha thaminiwa na kuondosha mali chakavu kwa mujibu wa Sheria na Kanuni za Fedha.  Aidha, kazi ya kuhakiki mali ya Serikali katika Wizara, Idara zinazojitegemea na Balozi za Tanzania nchi za nje itaendelea ili kutoa ushauri  na kuhakikisha kuwa mali ya Serikali inatunzwa na kutumika kwa malengo yaliyokusudiwa. Vile vile, Wizara itaandaa Sera ya Taifa ya Usimamizi wa Mali ya Serikali.

Usimamizi wa Mashirika na Taasisi za Umma
Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2011/12, Wizara imeendelea kusimamia utendaji wa Mashirika ya Umma pamoja na Taasisi za Serikali. Majukumu yaliyotekelezwa ni pamoja na: kuendesha zoezi la ukaguzi wa kimenejimenti katika Taasisi zifuatazo: Hospitali ya Rufaa KCMC, Chuo cha Ubaharia cha Dar es salaam (DMI), Tume ya Matumizi Bora ya Ardhi na Chuo Kikuu Kishiriki cha Stadi za Ushirika na Biashara (MUCCoBS). Aidha, uhakiki wa Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), Mamlaka ya Ustawishaji wa Makao Makuu (CDA), Shrika la Usimamizi na Ukaguzi wa vyama vya Ushirika (COASCO), Taasisi ya Uhasibu Arusha (IAA), Taasisi ya Utafiti wa madawa ya wadudu Waharibifu katika Nchi za Tropiki (TPRI), Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT), Taasisi ya uhandisi na Usanifu Mitambo (TEMDO) na kituo cha Zana za Kilimo na Teknolojia Vijijini (CAMARTEC) unaendelea kufanyika. Katika uhakiki huo masuala ya msingi yaliyoangaliwa ni pamoja na uzingatiaji wa Kanuni, Sheria na miongozo mbalimbali inayotolewa na Serikali, uwajibikaji na utawala bora, matumizi ya Fedha za Mishahara, Matumizi mengineyo na kuangalia jinsi taratibu za ajira zinavyozingatiwa katika Taasisi na Mashirika ya Umma. Zoezi hili ni endelevu na linalenga kuboresha uendeshaji wa Mashirika na Taasisi za Serikali.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2012/13, Wizara itatekeleza yafuatayo: kuchambua Bajeti za Mashirika na kuainisha kiasi cha mapato kinachoweza kupatikana kutoka katika kila Shirika ili yaweze kuchangia katika Mfuko Mkuu wa Serikali; kufanya ukaguzi wa Kimenejimenti (Management Audit) kwa Wakala, Taasisi na Mashirika ya Umma; kuchambua na kuidhinisha Miundo ya Utumishi na Mifumo ya Mishahara, Kanuni za Utumishi pamoja na Mikataba ya Hiari kwa Taasisi.

Mheshimiwa Spika, Wizara itasimamia na kuratibu zoezi la ubinafsishaji, urekebishaji na ufuatiliaji linaloendelea kwa Mashirika na Makampuni ya UDA, TRL, TTCL, ATCL, General Tyre East Africa, URAFIKI (FTC), na hisa za Serikali katika TDFL. Aidha, wizara itaimarisha Ofisi ya Msajili wa Hazina ili iweze kusimamia kikamilifu Mashirika ya Umma ikiwa ni pamoja na kutunga Sheria mpya ili kuipa nguvu zaidi za kusimamia mashirika na Taasisi za umma. 

Ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi – Public Private Partnership (PPP)

Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2011/12, Wizara imetayarisha  mwongozo wa uendeshaji wa miradi ya Ubia (PPP Operational Guidelines). Aidha, Wizara kwa kushirikiana na Ofisi ya Waziri Mkuu, imeandaa Mkakati wa Ubia kati ya sekta ya umma na sekta binafsi (PPP Implementation Strategy). Vile vile, wizara imeendelea kuimarisha kitengo kinachoshughulikia ubia kwa kuwapatia mafunzo maafisa walioko katika kitengo hicho pamoja na kuongeza vitendea kazi.

Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2012/13, Wizara imelenga kutoa mafunzo kuhusu dhana ya ubia kwa watumishi wa vitengo na madawati ya ubia katika wizara mbalimbali; kufanya utafiti wa baadhi ya miradi ya PPP ambayo inaendelea na kuanza kutathmini miradi ya ubia kwa lengo la kuidhinisha; na kukamilisha miongozo na taratibu za utekelezaji wa sera ya ubia pamoja na kusambaza kwa wadau.
Uratibu wa Utekelezaji wa MKUKUTA

Mheshimiwa Spika, MKUKUTA ni Mkakati wa Kitaifa wa Kukuza Uchumi na Kupunguza Umaskini, unaojielekeza katika matokeo katika maeneo makuu matatu, ambayo ni kukuza uchumi na Kupunguza Umaskini wa Kipato, Kuboresha Maisha na Ustawi wa Jamii na Utawala Bora na Uwajibikaji. Lengo likiwa kupunguza umaskini wa kipato kufikia asilimia 20.4 ifikapo mwaka 2015 kutoka asilimia 33.6 mwaka 2007. Utekelezaji wa MKUKUTA huratibiwa na Wizara kupitia Mpango wa Ufuatiliaji na Tathmini (MKUKUTA Monitoring Master Plan), na taarifa mbalimbali za uchambuzi wa utekelzaji hutolewa. Katika kipindi cha mwaka 2011/12 Wizara iliandaa na kusambaza Taarifa ya Mwaka ya Utekelezaji ya MKUKUTA, na  Taarifa ya Hali ya Umaskini na Maendeleo ya Watu, na Taarifa ya Maendeleo ya Malengo ya Millenia. Taarifa hizi zimechambua mwenendo wa viashiria vya umaskini, mafanikio, changamoto na zimependeka hatua za kuchukua. Aidha; wizara imekamilisha mkakati wa  mawasiliano wa MKUKUTA na utafiti wa maoni ya watu kuhusu umaskini (Views of the People Survey). Taarifa ya matokeo ya utafiti huo inaandaliwa.

Mheshimiwa Spika, jitihada nyingine zilizofanyika ni pamoja na kuhamasisha na kuelimisha umma kuhusu kukuza uchumi na kupunguza umaskini. Shughuli hizi ni pamoja na kuendesha semina kwa makundi mbalimbali ya kijamii, kuchapisha na kusambaza taarifa na majarida mbalimbali yenye lengo la kuhamasisha shughuli za uzalishaji na biashara.

Mradi wa Kutoa Mikopo kwa Wajasiriamali Wadogo (Small Entrepreneurs Loan Facility –SELF)
Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2011/12 Mfuko wa SELF ulitoa mikopo ya shilingi bilioni 8.77  kwa taasisi ndogo za fedha 111 na kuwafikia walengwa 7,729. Kwa wastani urejeshwaji wa mikopo ulifikia shilingi bilioni 8.31 ambazo ni sawa na asilimia 91.6. Aidha mafunzo yalitolewa kwa wajasiriamali 1,417, watendaji 317 ambao ni asilimia 99 ya walengwa (320), wakiwemo Maafisa mikopo, wajumbe wa kamati za mikopo za asasi, watunza vitabu vya fedha na wajumbe wa bodi, na watoa huduma za maendeleo ya biashara 39 ambao ni Maafisa Ushirika wa wilaya.

Programu ya Taifa ya Kuongeza Kipato (National Income Generation Programme – NIGP)

Mheshimiwa Spika, Programu ya Taifa ya Kuongeza Kipato ilikuwa na miradi mingi ya masoko na baba na mama lishe ambayo baadae ilikabidhiwa kwenye Mamlaka ya Serikali za Mitaa na kubakiza miradi michache ya ufugaji nyuki na kuzalisha chumvi. Katika mwaka 2011/12, Wizara iliendelea kusimamia NIGP kwa kufuatilia utekelezaji wa miradi hiyo. Wananchi walipatiwa mafunzo ya mbinu bora za ufugaji nyuki na miradi inayoendelea iliimarishwa kwa kupatiwa vifaa vya kuzalisha na kuvuna asali. Aidha NIGP iliendelea kusimamia miradi ya uzalishaji wa chumvi katika maeneo ya Chake Chake (Pemba) na Chukwani (Unguja).

Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2012/13, Wizara imelenga kutekeleza yafuatayo: kufanya tathmini ya MKUKUTA II na kuandaa taarifa ya mwaka ya utekelezaji ambayo itabainisha mafanikio na changamoto zilizopo; kuandaa Taarifa ya Malengo ya Milenia; kutambua na kuainisha juhudi mbalimbali za kinga ya jamii zinazofanyika nchini; na kutangaza fursa zinazotolewa na mifuko ya wajasiriamali (SELF na NIGP) kwenye vyombo vya habari ili wananchi waweze kunufaika nazo. Aidha, Wizara itafanya tathmini ya miradi ya programu ya NIGP ili kubaini namna bora ya utekelezaji.

Huduma kwa Wastaafu na Mirathi
Mheshimiwa Spika, pamoja na kuanzishwa kwa Mfuko wa Pensheni kwa Watumishi wa Umma (PSPF), Wizara ya Fedha inawalipa pensheni watumishi waliostaafu kabla ya Juni 2004, Wanajeshi, Usalama wa Taifa, Viongozi Wastaafu wa Kitaifa na watumishi wenye ajira katika Mamlaka mbili. Katika kipindi cha Julai 2011 hadi Juni 2012, Wizara imelipa mafao na stahili za wastaafu  ya shilingi bilioni 120.03 sawa na asilimia 100 ya bajeti iliyotengwa kwa mwaka wa fedha 2011/12. Wizara imeanza kuwalipa wastaafu pensheni kwa vipindi vya miezi mitatu mitatu badala ya miezi sita kuanzia Januari 2012. Aidha, Wizara inaendelea kuweka kumbukumbu zilizopo kwenye majalada binafsi ya wastaafu kwenye mfumo wa kompyuta ujulikanao kwa jina la Saperion kwa lengo la kurahisisha upatikanaji  wa taarifa za mstaafu.

Mheshimiwa Spika, Wizara imechukua hatua mbali mbali zenye lengo la kuondoa ucheleweshaji wa malipo ya mirathi. Hatua zilizochukuliwa na Wizara ni pamoja na: kutoa elimu kwa umma kupitia vipeperushi, maonesho mbalimbali ya kitaifa; kutoa mafunzo kwa maafisa wa ofisi za HAZINA ndogo na Makarani na Wahasibu wa Mahakama zinazoshughulikia malipo ya mirathi ambayo yalifanyika katika kanda sita zenye Mikoa minne minne katika vituo vya Mwanza, Arusha, Dodoma, Morogoro, Mbeya na Dar es Salaam.

Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2012/13, Wizara itatoa mafunzo kama hayo kwa baadhi ya Mahakimu kutoka katika mahakama zinazoshughulikia malipo ya mirathi ili kuwepo na uelewa sawa kwa maafisa wa mahakama hizo.

Michango ya Mwajiri katika Mifuko ya Hifadhi ya Jamii.

Mheshimiwa Spika, Wizara imeendelea kuwasilisha michango ya mwajiri ya watumishi wa Serikali kuu na Serikali za mitaa kwenye mifuko mbalimbali ya hifadhi ya jamii (PSPF, GEPF, LAPF, PPF na NSSF), pamoja na Mfuko wa Bima ya Afya -NHIF. Kufikia mwezi Juni 2012  kiasi cha shilingi bilioni 534.0 kimewasilishwa kwenye mifuko hiyo.  Katika mwaka wa fedha 2012/13, Wizara itaendelea kulipa michango ya mwajiri kwa mujibu wa sheria kwa watumishi wa Serikali Kuu na Serikali za Mitaa kila mwezi kwenye Mifuko ya Hifadhi ya Jamii na Bima ya Afya.


Sheria na Miswada ya Fedha
Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2011/12 wizara iliendelea kuzifanyia marekebisho sheria mbalimbali ili ziendane na wakati. Baadhi ya sheria zilizofanyiwa marekebisho ni Sheria ya Fedha Haramu Sura 423 (The Anti-Money Laundering (Amendment) Act, 2012) ambayo ilipitishwa na Bunge mwezi Februari, 2012 pamoja na  Sheria ya Fedha ya mwaka 2011 (The Finance Act, 2011). Aidha, Sheria ya Ununuzi wa Umma ya mwaka 2011 ilipitishwa na Bunge mwezi Novemba 2011. Vile vile, Sheria ya Bima ya mwaka 2009 ilifanyiwa marekebisho na Bunge mwezi Aprili 2012.

Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2012/13,   Wizara           itaendelea kukamilisha maandalizi ya kuwezesha kutungwa kwa Sheria ya Usimamizi wa Malipo ya Ki-elektroniki (The National Electronic Payment System Act).  Maandalizi ya pili ni Sheria ya Usimamizi wa Taasisi zinazotoa Mikopo Midogo Midogo (The National Microfinance Act). Sheria hii inalenga kuvitambua vikundi kama VIKOBA na Taasisi nyingine ndogo ndogo.  Serikali itakapokamilisha maandalizi ya sheria hizi itawasilisha miswada ya sheria husika kwa ajili ya kujadiliwa hapa bungeni. Aidha, Wizara itaendelea kuandaa Kanuni za Sheria mbalimbali za fedha pamoja na nyaraka za kisheria.  Juhudi hizi zitasaidia Sheria hii kurasimisha makundi hayo na hivyo kuleta msukumo wa kiuchumi katika jamii.

Masuala ya Watumishi
Mheshimiwa Spika, katika jitihada za kuongeza ufanisi Wizara imefanya yafuatayo: imeajiri watumishi 57 wa kada mbalimbali; imebadilisha kada watumishi 17; imethibitisha kazini watumishi 229 wa kada mbalimbali; na kupandisha vyeo watumishi 214. Aidha, Wizara imeendelea kuboresha utendaji wa watumishi wake kwa kuwapatia mafunzo ya muda mfupi na mrefu. Vile vile, katika kutekeleza mkakati wa kupambana na ukimwi, Wizara imehudumia watumishi wanaoishi na virusi vya ukimwi. Wizara pia ilifanya vipimo kwa watumishi kwa magonjwa ya saratani na kisukari. Kadhalika, katika kujenga afya za watumishi wizara imekuwa ikitoa fursa kwa watumishi kushiriki katika michezo mbalimbali.

Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2012/13, wizara imepanga kutekeleza yafuatayo: kuajiri watumishi 80 wa kada mbalimbali; kubadilisha kazi watumishi waliopata sifa mbalimbali za kitaaluma; kuthibitisha watumishi kazini waliomaliza muda wao wa majaribio; na kupandisha vyeo watumishi 300. Aidha, Wizara itaendelea kuwapatia watumishi  wake mafunzo mbalimbali ya kuwajengea uwezo katika kutekeleza majukumu yao. Vile vile, wizara itaendelea kutoa elimu kuhusu magonjwa sugu pamoja na kuwapatia lishe walioathirika na ukimwi.

Usimamizi na Uratibu wa Miradi  na Shughuli za Wizara
Mheshimiwa Spika, Wizara imesimamia na kuratibu utekelezaji wa miradi ya maendeleo iliyo chini yake. Miradi hiyo ni pamoja na: Ujenzi wa Ofisi ya  HAZINA na Upanuzi wa Chuo cha Mipango na Maendeleo Vijijini – Dodoma; Ujenzi wa Maktaba – Chuo cha Uhasibu - Arusha; Ujenzi wa Kituo cha Taaluma ya Uhasibu - Dar es Salaam; na Ukarabati wa majengo ya Chuo cha Usimamizi wa Fedha; na Chuo cha Takwimu Mashariki mwa Afrika.

Mheshimiwa Spika, Wizara iliratibu utekelezaji wa Programu ya Maboresho ya Usimamizi wa Fedha za Umma (Public Finance Management Reform Programme- PFMRP), ambayo utekelezaji wake umeingia katika awamu ya nne kuanzia mwezi Julai 2012. Maeneo yaliyolengwa katika awamu hiyo ni: Usimamizi wa Mapato ya Serikali; Mipango na Uandaaji wa bajeti ya Serikali; Utekelezaji wa Bajeti; Uwazi na Uwajibikaji; Udhibiti wa Bajeti ya Serikali na Ufuatiliaji na Tathmini; na Usimamizi wa Programu na Mabadiliko ya Utendaji. Aidha, Wizara pia imekamilisha uhuishaji wa Mpango Mkakati wake wa miaka mitano (2012/13 – 2016/17), pamoja na  Mkataba wa Huduma kwa Mteja ambayo imeanza kutekelezwa katika mwaka wa fedha 2012/13 .
Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2012/13, wizara itaendelea kusimamia Utekelezaji wa Mpango Mkakati wa Wizara pamoja na kutekeleza Mpango Mkakati wa awamu ya nne ya Programu ya Maboresho ya Usimamizi wa Fedha za Umma (PFMRP IV).

Miradi ya Millenium Challenge Corporation (MCC)
Mheshimiwa Spika, Wizara imesimamia utekelezaji wa miradi inayofadhiliwa na Serikali ya Marekani kupitia MCC ikijumuisha Miradi ya Barabara ya Tunduma-Sumbawanga, Songea-Namtumbo, Peramiho – Mbinga na Tanga - Horohoro; barabara za vijijini Pemba; na Kiwanja cha ndege cha Mafia. Mradi wa barabara ya Tanga - Horohoro upo katika hatua za mwisho za kukamilishwa. Miradi mingine ni ya nishati na maji ambayo utekelezaji wake upo katika hatua mbalimbali. Miradi ya nishati inajumuisha kutandika waya wa umeme chini ya bahari kwenda Zanzibar; kukarabati vituo 24 vya umeme; upanuzi wa mtandao wa umeme katika mikoa ya Tanga, Morogoro, Iringa, Mbeya, Dodoma, Mwanza na Kigoma. Aidha, Miradi ya maji inayotekelezwa ni: upanuzi wa mtambo wa kuchuja maji wa Ruvu Chini; na ukarabati wa mifumo ya maji ya Manispaa ya Morogoro na  Jiji la Dar es Salaam.

Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2012/13, Wizara itakamilisha miradi ya MCC na kukabidhi miradi iliyokamilika kwa taasisi husika pamoja na kutoa mafunzo kwa ajili ya kuhakikisha usimamizi endelevu wa miradi hiyo.

Tume ya Pamoja ya Fedha (Joint Finance Commission – JFC)

Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2011/12, Tume ya Pamoja ya Fedha imekamilisha Utafiti wa usimamizi wa deni la taifa linalohusu Serikali mbili na kufanya utafiti wa  kubaini mfumo bora wa kodi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.  Matokeo ya tafiti hizo yatawasilishwa kwenye ngazi husika. Aidha, ili kuiwezesha Tume kufanya kazi kwa ufanisi, imepewa fungu lake la kibajeti.

Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2012/13 Wizara kupitia Tume ya Pamoja ya Fedha imepanga kukamilisha utafiti wa mfumo wa kodi wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kuanzisha programu ya kutekeleza sera ya Taifa ya Mfumo wa habari na mawasiliano na kutoa ushauri kuhusu ushirikishwaji wa pande mbili za Muungano katika utafutaji wa Misaada na Mikopo.



Udhibiti wa Fedha Haramu na Ufadhili wa Ugaidi

Mheshimiwa Spika, Sheria ya Udhibiti wa Fedha Haramu inazitaka benki na taasisi za fedha kutunza kumbukumbu sahihi kuhusu wateja wake. Katika kutekeleza jukumu hili, benki na taasisi za fedha zilitakiwa  kuhuisha taarifa zote za wateja wake kufikia Machi 2012. Kwa kuwa kumbukumbu hizi zilihusu kipindi kirefu sana na idadi kubwa ya wateja, benki ziliomba kuongezewa muda hadi Machi 2013 ili ziweze kukamilisha zoezi la kuhakiki taarifa za wateja wake.

Mheshimiwa Spika, Wizara kupitia kitengo cha Udhibiti wa Fedha Haramu na Ufadhili wa Ugaidi (Financial Intelligence Unit - FIU)  imetoa mafunzo ya Udhibiti wa Fedha Haramu na Ufadhili wa Ugaidi kwa wafanyakazi wa Kitengo. Mafunzo hayo yametolewa pia kwa  Jeshi la Polisi, Mamlaka ya Mapato, TAKUKURU na Kurugenzi ya Mashtaka.  Aidha, mafunzo mengine ya  kupiga vita fedha haramu yalitolewa kwa baadhi ya wafanyakazi  wa benki, mashirika ya bima, kasino na biashara za michezo ya kubahatisha, makampuni ya simu, masoko ya mitaji na hisa, waandishi wa habari, mahakimu, majaji, na wanasheria. 

Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2012/13, wizara itafanya yafuatayo: kuboresha Mkakati wa kitaifa wa kupambana na fedha haramu na ufadhili wa ugaidi; kutoa elimu ya kupiga vita fedha haramu na ufadhili wa ugaidi; na kuandaa kanuni, miongozo na taratibu za kukagua watoa taarifa, kwa kushirikiana na wasimamizi wa watoa taarifa. 

Habari, Elimu na Mawasiliano kwa Umma

Mheshimiwa Spika, Wizara ilisimamia na kuendelea kuboresha mawasiliano kati yake na wadau kwa kutoa taarifa kwa wakati. Katika kipindi cha mwaka wa fedha 2011/12, elimu kwa umma imetolewa kwa wananchi kuhusu majukumu, mafanikio na changamoto za Wizara  kupitia machapisho na vyombo vya habari na njia mbalimbali yakiwemo Magazeti, Redio, Tovuti, Televisheni na vipeperushi. Aidha, Wizara imeendelea kuhamasisha umma kuhusu umuhimu wa kushiriki katika zoezi la sensa ya watu na makazi.  

Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2012/13, wizara itatoa elimu kuhusu utendaji wa Wizara, utaratibu wa malipo kwa wastaafu, sheria za kodi na taratibu za kukata rufani.


Ununuzi wa Umma

Mheshimiwa Spika, katika eneo la Ununuzi wa Umma, Wizara imetekeleza majukumu yafuatayo: kusimamia marekebisho ya Sheria ya Ununuzi wa Umma ya  mwaka 2004; kuandaa Kanuni za Ununuzi wa Umma; kusimamia uandaaji wa Sera ya Taifa ya Ununuzi wa Umma; na kusimamia na kuendeleza kada ya Ununuzi na Ugavi Serikalini. Vile vile, Wizara imeboresha daftari la Maafisa Ununuzi na Ugavi Serikalini kwa lengo la kuwatambua na sifa zao.

Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2012/13, Wizara inalenga kutekeleza yafuatayo: kukamilisha uandaaji wa Sera ya Ununuzi wa Umma; kuhakikisha ununuzi wa umma unatekelezwa kwa kuzingatia sheria na kuendelea kuhuisha daftari la maofisa ununuzi  na ugavi serikalini. Aidha, wizara itafanya uchambuzi wa wataalamu wa ununuzi na ugavi ili kubaini mahitaji halisi na kuongeza udahili wa wanafunzi wa taaluma hii katika vyuo vyetu.

Udhibiti wa Ununuzi wa Umma
Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2011/12, Wizara kupitia Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (Public Procurement Regulatory Authority - PPRA) ilitekeleza yafuatayo:  kutoa mafunzo kwa taasisi za ununuzi 18 zikiwemo Halmashauri na kuhudhuriwa na watumishi 370 kwa lengo la kuboresha ununuzi kwenye Halmashauri na taasisi nyingine ambazo zilikuwa na hoja mbalimbali za ukaguzi; kuandaa warsha ya wakuu wa vitengo vya ununuzi nchini ambayo ilihudhuriwa na wakuu wa vitengo vya ununuzi 184; na kutoa mafunzo kwa wataalamu wa ununuzi 10 kutoka PPRA kuhusu mbinu za kugundua rushwa katika ununuzi wa umma na kufanya ukaguzi wa kiutambuzi. 

Mheshimiwa Spika, PPRA imeendendelea kuelimisha umma na kutoa taarifa za zabuni mbalimbali za Taasisi za Umma kupitia jarida la ununuzi – Tanzania Procurement Journal litolewalo kila wiki na tovuti ya PPRA (http://www.ppra.go.tz); kuandaa program ya uelimishaji umma kuhusu masuala ya ununuzi; na kutoa mafunzo kwa taasisi 46 kuhusu matumizi ya mfumo wa upokeaji na usimamizi wa taarifa za ununuzi nchini.

Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2012/13, Wizara imelenga kuongeza ufanisi wa usimamizi na udhibiti wa ununuzi wa umma kulingana na sheria mpya ya ununuzi wa umma kwa kufanya yafuatayo: kuanza maandalizi ya kujenga ofisi za kudumu za PPRA na kuajiri watumishi wa kutosha; na kufungua ofisi za kanda ili kuiwezesha PPRA kupanua wigo wa usimamizi na ukaguzi kwenye taasisi zilizopo mikoani hususan Halmashauri.

Rufaa za Zabuni za Umma
Mheshimiwa Spika, katika mwaka fedha 2011/12, jumla ya rufaa 12 zilipokelewa na Mamlaka ya Rufaa za Zabuni za Umma (Public Procurement Appeals Authority – PPAA) na kutolewa maamuzi. Aidha, Mamlaka iliendesha warsha saba za kuelimisha Wazabuni na watendaji wa Serikali na Taasisi za Umma juu ya Sheria ya Ununuzi wa Umma hususan, taratibu za uwasilishaji malalamiko pamoja na haki na wajibu wao katika kuimarisha usimamizi wa shughuli za ununuzi wa umma. Warsha hizo zilifanyika Singida, Shinyanga, Babati, Karatu na Arusha.

Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2012/13, Mamlaka itatekeleza majukumu yafuatayo: kuendelea kushughulikia migogoro inayojitokeza katika ununuzi wa umma; kutoa elimu kwa Wazabuni, Watendaji wa Serikali na Taasisi zake pamoja na umma kwa ujumla juu ya Sheria mpya ya ununuzi wa Umma ya mwaka 2011; na kujenga uwezo kwa watendaji na wajumbe wa Mamlaka juu ya utatuzi wa migogoro na ununuzi katika miradi ya ubia kati ya sekta ya umma na binafsi.

Huduma ya Ununuzi Serikalini 
Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2011/12, Wizara kupitia Wakala wa Huduma ya Ununuzi Serikalini (Government Procurement Services Agency – GPSA) ilitekeleza majukumu yafuatayo: kuanza utaratibu wa kusimika mfumo wa matumizi ya ‘smart card’ kwa ajili ya ununuzi wa mafuta wenye tija kwa magari ya Serikali ambapo mkandarasi amepatikana; kuendesha mafunzo kuhusu mfumo wa ununuzi wa vifaa na huduma mtambuka unavyofanya kazi kwa lengo la kuwajengea weledi watumishi wa umma na wafanyabiashara katika kituo cha Mwanza ambapo washiriki walitoka mikoa ya Mwanza, Dar es Salaam, Dodoma, Shinyanga, Kigoma, Kagera, Mara na Tabora. Aidha, wakala umekamilisha ukarabati na upanuzi wa kisima cha mafuta cha Dar es Salaam na ukarabati wa ofisi ya Tanga. Ukarabati na ujenzi wa ofisi na visima vya mafuta katika mikoa ya Tabora, Shinyanga, Lindi, Mtwara, Dodoma na Manyara unaendelea.


Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2012/13, Wizara imepanga kutekeleza yafuatayo: Kufungua ofisi za kutoa huduma ya uuzaji wa mafuta na vifaa vya ofisi kwenye mikoa mipya ya Njombe, Katavi, Geita na Simiyu; kutoa mafunzo kwa watumishi wa umma na wafanyabiashara kuhusu mfumo wa ununuzi wa vifaa na huduma mtambuka; kukamilisha ujenzi na ukarabati wa ofisi, maghala na vituo vya mafuta katika mikoa ya Manyara, Dodoma, Dar es Salaam, Kilimanjaro, Tabora, Mbeya, Morogoro, Shinyanga, Lindi, Mtwara, Rukwa na Mwanza na kusimika mitambo ya usimamizi wa usalama (CCTV) wa mali za Wakala na wateja wake katika kituo cha mafuta cha Kurasini, Dar es Salaam.

Rufaa za Kodi 
Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2011/12, Bodi ya Rufaa za Kodi (Tax Revenue Appeals Board - TRAB) imepokea rufaa 107 na imesikiliza na kutolea maamuzi rufaa 79. Aidha,  Bodi imechapisha taarifa -  kwa rufaa zote zilizoamuliwa kuanzia mwaka 2005 – 2008- Tanzania Tax Law Reports. Vile vile, Wizara kupitia Baraza la Rufaa za Kodi (Tax Revenue Appeals Tribunal - TRAT) imepokea rufaa  44 ambapo rufani 31 zimesikilizwa na kutolewa maamuzi. Kadhalika, Baraza limetoa elimu kwa walipa kodi kuhusu taratibu za kukata rufaa ya kodi na sheria za kodi katika mkoa wa Kagera.


Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2012/13, wizara kupitia Bodi ya rufaa za kodi imepanga kufanya yafuatayo: kusikiliza na kutolea maamuzi rufaa 103; kutoa elimu kwa walipa kodi juu ya taratibu za kukata rufaa za kodi katika kanda ya kaskazini; kutoa mafunzo kwa wajumbe wapya wa Bodi juu ya taratibu za kutatua migogoro ya kodi itokanayo na sheria za kodi zinazosimamiwa na Mamlaka ya Mapato Tanzania na kuchapisha Tanzania Tax Law Reports  za mwaka 2009-2010. Aidha, wizara kupitia Baraza la Rufaa za Kodi inategemea kupokea, kusikiliza na kutolea maamuzi rufaa 80; kutoa elimu kwa walipa kodi katika mikoa  ya Manyara, Dodoma, Singida na Mbeya juu ya taratibu za kukata  rufaa za kodi.

Mamlaka ya Mapato Tanzania – TRA
Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2011/12, Mamlaka ya Mapato Tanzania, ambayo ni wakala wa serikali wa ukusanyaji wa mapato ya kodi imeendelea na jukumu hilo. Lengo la makusanyo kwa mwaka 2011/12 lilikuwa ni shilingi bilioni 6,228.8. Hadi Juni, 2012 jumla ya shilingi bilioni 6,511.2. zilikusanywa ikiwa ni sawa na asilimia 104.5 ya lengo. Katika mwaka wa fedha 2012/13 lengo ni kukusanya shilingi bilioni 8,070.09.

Mheshimiwa Spika, ili kufikia lengo hilo, Mamlaka ya Mapato Tanzania imepanga kuendelea kusimamia mikakati mbalimbali inayolenga kuboresha makusanyo ya mapato yatokanayo na kodi. Maeneo yatakayopewa kipaumbele ni pamoja na: Kuendelea kuimarisha matumizi ya mifumo ya ki-elektroniki katika utawala wa kodi ikiwa ni pamoja na kupanua wigo wa matumizi ya mashine za ki-elektroniki za kutoa stakabadhi za kodi (Electronic Fiscal Device – EFD) na mfumo wa kuwasilisha ritani (returns) za kodi kwa njia ya ki-elektroniki .

MIFUKO YA PENSHENI
Mfuko wa Pensheni kwa Watumishi wa Umma – PSPF
 Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2011/12, mfuko umeendelea kusajili na kuhifadhi kumbukumbu za wanachama pamoja na kukusanya michango na kuiwekeza. Aidha, Mfuko ulikusanya jumla ya shilingi bilioni 527.22 ambapo kati ya makusanyo hayo, michango ya wanachama ni shilingi bilioni 449.99 na mapato yatokanayo na vitega uchumi ni shilingi bilioni 77.23. Kati ya hizo, shilingi bilioni 371.40 zilitumika kulipa mafao ikiwa ni pamoja na mafao ya kiinua mgongo na pensheni za kila mwezi.

Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha  2012/13, Mfuko unatarajia kukusanya jumla ya shilingi bilioni 718.30. Kati ya hizo, michango ya wanachama ni shilingi bilioni 590.19 na mapato yatokanayo na vitega uchumi ni shilingi bilioni 128.11. Mfuko unatarajia kulipa kiasi cha shilingi bilioni 452.93 kwa ajili ya mafao mbalimbali ikiwa ni pamoja na kiinua mgongo na pensheni za kila mwezi ambapo jumla ya wanachama 6,974 wanatarajia kustaafu kwa mujibu wa sheria.

Mheshimiwa Spika, Hadi tarehe 30 Juni 2012, Mfuko ulikuwa na thamani ya shilingi bilioni 1,071.19. Mfuko unatarajiwa kufikia thamani ya shilingi bilioni 1,438.29 ifikapo tarehe 30 Juni 2013. Ongezeko hili ni sawa na asilimia 34.27.

Mfuko wa Akiba ya Wafanyakazi Serikalini – GEPF
Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2011/12, Mfuko wa Akiba ya Wafanyakazi Serikalini (GEPF) ulitekeleza majukumu yake kwa mafanikio makubwa. Thamani ya Mfuko imeongezeka kutoka shilingi bilioni 119.4 mwezi Juni, 2011 hadi kufikia shilingi bilioni 150 mwezi Juni 2012. Mapato yatokanayo na vitega uchumi yameongezeka kutoka shilingi bilioni 9.4 mwaka 2010/11 hadi shilingi bilioni 10.9 kwa mwaka 2011/12. Aidha, Mfuko umesajili wanachama wapya 10,401 kupitia mpango wa lazima na mpango wa hiari ambapo umeyafikia makundi mbalimbali ya wazalishaji mali wakiwemo wakulima, wafanyabiashara, wasafirishaji, wafugaji na waajiriwa. Mafanikio haya yametokana na juhudi za kuutangaza mfuko kupitia vyombo mbalimbali vya habari. 

Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2012/13, Mfuko utaendelea kuboresha huduma kwa wanachama, kupanua wigo wa wanachama, kukuza mapato yatokanayo na uwekezaji na kusajili wanachama zaidi kupitia skimu zote mbili ambazo ni Teknolojia ya Habari na Mawasiliano pamoja na kuimarisha mpango wa hiari wa kujiwekea akiba ya uzeeni kwa kufungua ofisi tatu katika Manispaa za Dar es Salaam na kuimarisha ofisi zilizopo mikoani. Lengo ni kusajili jumla ya wanachama 19,606 na kukusanya michango inayofikia shilingi bilioni 35.21 ifikapo mwezi Juni, 2013. Vile vile, mapato yatokanayo na vitega uchumi yanatarajiwa kufikia shilingi bilioni 16 na thamani ya mfuko kufikia shilingi bilioni 200. 

Mfuko wa Pensheni wa Mashirika ya Umma – PPF
Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2011, Mfuko wa Pensheni wa mashirika ya umma – Parastatal Pension Fund (PPF), ulikusanya shilingi bilioni 188.1, ikiwa ni michango ya wanachama ambayo ni ongezeko la asilimia 27 ikilinganishwa na shilingi bilioni 147.65 zilizokusanywa mwaka 2010.  Katika kipindi cha Januari – Juni 2012, Mfuko ulikuwa umekusanya shilingi bilioni 112.3,  ikiwa ni michango kutoka kwa wanachama. Kadhalika, mapato yatokanayo na uwekezaji yaliongezeka kutoka shilingi bilioni 35.2 mwaka 2010 hadi shilingi bilioni 88.1 mwaka 2011, ikiwa ni ongezeko la asilimia 140.

Mheshimiwa Spika, idadi ya wanachama wanaochangia katika Mfuko imeongezeka kutoka 160,068 mwaka 2010 hadi kufikia wanachama 180,049 mwaka 2011. Mfuko umelipa jumla ya shilingi bilioni 71.9 kwa mwaka 2011, ikiwa ni ongezeko la asilimia 12.7 ikilinganishwa na shilingi bilioni 63.8 zilizolipwa mwaka 2010. Aidha, kufikia Desemba 2011, thamani ya Mfuko ilikuwa shilingi bilioni 896.1, ikiwa ni ongezeko la asilimia 24 ikilinganishwa na shilingi bilioni 722.47 mwezi Desemba 2010. Vile vile, thamani ya Mfuko hadi kufikia Juni, 2012 ilikuwa imefikia shilingi bilioni 989. 

Mheshimiwa Spika, kwa mwaka 2013, Mfuko umejiwekea malengo ya kukusanya michango kutoka kwa wanachama ya kiasi cha shilingi bilioni 244 na mapato yatokanayo na uwekezaji ya shilingi bilioni 103.5 ili kuwezesha thamani ya mfuko kukua hadi kufikia shilingi bilioni 1,220.6 kutoka shilingi bilioni 1,058.7 mwaka 2012. Mfuko unatarajia kulipa mafao ya jumla ya shilingi bilioni 84.6 ifikapo mwishoni mwa mwaka 2013. Aidha, Mfuko unategemea kuandikisha jumla ya wanachama 55,000 kutoka katika sekta ya Umma na binafsi.

HUDUMA ZA KIBENKI
Benki Kuu ya Tanzania

 Mheshimiwa Spika, Sekta ya benki imeendelea kuwa imara, na benki nyingi zimekuwa na mitaji ya kutosha (capital adequecy) pamoja na viwango vya juu vya ukwasi (liquidity), ikilinganishwa na viwango vinavyotakiwa kulingana na kanuni (prudential guidelines).  Uwiano wa mtaji na mali iliyowekezwa (core capital to total risk weighted assets and off-balance sheet exposures) ulikuwa asilimia 17.5 mwezi Juni 2012 ikilinganishwa na kiwango cha chini kinachotakiwa kisheria cha asilimia 10.0.  Uwiano kati ya mikopo na amana za wateja (credit/deposit ratio) ulikuwa  asilimia 67.5, ikilinganishwa na kikomo cha asilimia 80.0. Vile vile, uwiano kati ya mikopo chechefu na jumla ya mikopo (non performing loans/total loans) yote katika mabenki ulipungua hadi kufikia asilimia 8.2 mwezi Juni 2012 kutoka asilimia 9.1 mwezi Juni 2011.  Hali hii ni kithibitisho cha uboreshaji wa urudishaji mzuri wa mikopo itolewayo na mabenki.

Mheshimiwa Spika, Benki Kuu imeimarisha na kuboresha mfumo wa malipo baina ya mabenki (Tanzania Inter-bank Settlement System – TISS) kwa kujumuisha malipo ya fedha za kigeni kupitia mfumo huu. Aidha, Bodi ya Mapato ya Zanzibar na Mamlaka ya Mapato Tanzania kwa upande wa Zanzibar zilianza kutumia mfumo huo. Hali hii ilisaidia kupunguza matumizi ya hundi za Serikali kutoka hundi 79,803 zenye thamani ya Shilingi bilioni 6,275.3 hadi hundi 55,838 zenye thamani ya Shilingi bilioni 6,115.6. Vile vile, Benki Kuu imeanza kutumia mfumo wa malipo kwa njia ya elektroniki.

Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2012/13, Wizara kwa kushirikiana na Benki Kuu imepanga kutekeleza sera ya fedha yenye lengo la ukuaji wa wastani wa fedha ya msingi usiozidi asilimia 16.0 na wa ujazi wa fedha kwa tafsiri pana zaidi (M3) usiozidi asilimia 18.0, ili kutoa nafasi kwa mikopo kwa sekta binafsi kukua kwa asilimia 20.0. Aidha,  Benki Kuu itatekeleza yafuatayo: kusimamia sekta ya fedha kwa lengo la kuhakikisha kuwa inaimarika kwa kuanzisha kiungo muhimu cha kuimarisha ushirikiano katika usimamizi na ufuatiliaji wa majanga mbalimbali katika mfumo wa kibenki; kutoa miongozo ya kuimarisha usimamizi wa huduma za kibenki kwa njia ya simu za mkononi nchini ili kuongeza ufanisi katika huduma ya malipo; na kuongeza biashara kati ya Nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki kupitia Mfumo wa Malipo wa Afrika Mashariki.

Benki ya Rasilimali Tanzania – TIB
 Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2011/12 Wizara imeendelea kuimarisha Benki ya Rasilimali kwa kutekeleza yafuatayo: kuanza utaratibu wa utekelezaji wa mfumo wa makampuni mawili yanayofanya kazi pamoja ambayo ni , kampuni mama - Benki ya Maendeleo na kampuni tanzu - Benki ya Biashara; kufungua tawi la benki Mbeya ambalo limeanza kazi   Mwezi Juni 2012 kwa lengo la kusogeza huduma karibu na wananchi. Aidha, katika kipindi kilichoishia Desemba 2011, Benki ya Rasilimali ilipata faida (kabla ya kodi) ya shilingi bilioni 5.8 ikiwa ni ongezeko la  shilingi bilioni 2.2 ikilinganishwa na mwaka ulioishia Desemba 2010. Vile vile, waraka mizania wa benki ulikua kufikia shilingi bilioni 305.8 ikilinganishwa na shilingi bilioni 243.7 Desemba 2010; Mikopo iliongezeka kufikia shilingi bilioni 181.7 kutoka shilingi bilioni 106.1 Desemba 2010.

Mheshimiwa Spika, kuanzia Julai 2011 hadi kufikia mwishoni mwa mwezi Juni 2012 Dirisha la Kilimo katika Benki ya Rasilimali lilitoa mikopo yenye thamani ya shilingi bilioni 14.23 na hivyo kufanya mikopo yote  kufikia shilingi bilioni 33.71. Kati ya mikopo iliyoidhinishwa shilingi bilioni 6.88 zilienda kwa vikundi vya wakulima wadogo na SACCOS, na hivyo kufanya jumla ya mikopo iliyotolewa kwa kundi hili kufikia shilingi bilioni 12.88, wakati shilingi bilioni 7.35 zilitolewa kwa makampuni na hivyo kufanya jumla ya mikopo iliyotolewa kwa kundi hili kufikia shilingi bilioni 15.35. Hadi mwezi Juni mwaka huu kiasi cha shilingi bilioni 2.76 ikijumuisha riba ya shilingi milioni 795.69 kilikuwa kimerejeshwa.

Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2012/13 Benki ya Rasilimali itatekeleza mpango mkakati wake ambao umelenga kuwezesha uwekezaji katika shughuli mbalimbali zikiwemo za madini, uvuvi, mifugo, miundombinu, utalii, viwanda hususan usindikaji wa mazao ya kilimo.  Aidha, wizara itaendelea kuongeza mtaji wa TIB kadri hali ya fedha itakavyoruhusu.

Benki ya Posta Tanzania – TPB
Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2011, Benki ya Posta imeendelea kuboresha huduma ambapo amana za wateja ziliongezeka kutoka shilingi milioni 107,327 mwaka 2010 na kufikia shilingi milioni 120,485 mwaka 2011, ikiwa ni ongezeko la asilimia 12.3. Aidha, idadi ya wateja iliongezeka kutoka 582,774 mwaka 2010 hadi kufikia 612,005 mwishoni mwa mwaka 2011. Thamani ya vitega uchumi vyote hadi Desemba 2011 iliongezeka na kufikia kiasi cha shilingi milioni 121,002 kutoka shilingi milioni 112,758 mwaka 2010, ikiwa ni ongezeko la asilimia 7.3. Vile vile, Benki iliendelea kutoa huduma za mikopo kwa wateja wake ambapo hadi kufikia Desemba 2011 uwekezaji kupitia mikopo ulikuwa na thamani ya jumla ya shilingi milioni 66,745 kutoka shilingi milioni 64,084 mwaka 2010, ikiwa ni ongezeko la asilimia 4.2.

Mheshimiwa Spika, katika kipindi hicho mapato yatokanayo na mikopo pamoja na  riba katika dhamana za Serikali yaliongezeka na kufikia shilingi milioni 24,276 ikilinganishwa na shilingi milioni 20,285 zilizopatikana mwaka 2010. Hili ni ongezeko la asilimia 19.7 na hivyo kufanya faida ya Benki baada ya kodi kuongezeka kutoka shilingi milioni 465 mwaka 2010 hadi shilingi milioni 2,267 mwaka 2011, ikiwa ni ongezeko la asilimia 387. Aidha, benki ilipata mapato kutokana na kuingia katika mkataba wa kukusanya kodi za ndani kwa niaba ya Mamlaka ya Mapato Tanzania.  

Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha  2012/13, Benki inalenga kutekeleza yafuatayo: kuimarisha matumizi ya teknolojia ya TPB Popote kwa huduma ya benki kupitia simu za mkononi  kwa lengo la  kuwafikia watanzania waishio vijijini; kuongeza idadi ya mikopo kwa kupanua wigo wa wateja ikiwa ni pamoja na kuingia mikataba na Halmashauri za Wilaya mbalimbali; na kuongeza mapato ya Benki kufikia shilingi milioni 28,621. Lengo ni kupata faida baada ya kodi isiyopungua shilingi milioni 3,563.

Twiga Bancorp Limited
Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha ulioishia tarehe 31 Desemba 2011, Twiga Bancorp Limited iliendelea kutoa huduma mbali mbali na kuweza kukusanya mapato ya shilingi bilioni 10.0, ikilinganishwa na mapato ya shilingi bilioni 9.6 kwa mwaka uliotangulia, ikiwa ni ongezeko la shilingi bilioni 0.4 sawa na  asilimia 4.1. Aidha, amana za wateja ziliongezeka kufikia shilingi bilioni 54.2 kwa kipindi kilichoishia Desemba 2011 kutoka shilingi bilioni 48.2 kama  ilivyokuwa Desemba 2010, ikiwa ni ongezeko la shilingi bilioni 6.0 sawa na asilimia 12.4. Mpaka kufikia Desemba, 2011 mikopo iliyotolewa na Twiga Bancorp Ltd kwa wateja mbalimbali ilifikia shilingi bilioni 35.9,  ikilinganishwa na shilingi bilioni 30.7 mwaka ulioishia Desemba 2010, ikiwa ni ongezeko la shilingi bilioni 5.2 sawa na asilimia 16.9. Vile vile, hadi kufikia Desemba 2011 Taasisi ilikuwa imewekeza shilingi bilioni 19.0 kwenye Dhamana za Serikali na Amana katika Benki zingine ikilinganishwa na shilingi bilioni 20.5 mwaka ulioishia Desemba 2010.

Mheshimiwa Spika, kwa mwaka utakaoishia Desemba 2012 Taasisi itatekeleza yafuatayo: kuimarisha huduma kwa kutumia Mashine za kutolea Pesa ‘ATMs’; kuongeza matawi katika mji wa Dodoma na Jiji la Dar es Salaam;  kuimarisha huduma mpya za kibiashara za kutoa mikopo kwa Sekta ya Viwanda na Biashara Ndogo na Kati pamoja na  mikopo ya kulipia Bima za wateja na kubadilisha Muundo wa Taasisi kuwa Benki Kamili.

Consolidated Holdings Corporation – CHC
 Mheshimiwa Spika, katika kipindi kilichoishia Desemba 2011 CHC ilikusanya mapato yaliyofikia shillingi bilioni 6.3 sawa na asilimia 66 ya lengo.  Upungufu huu wa mapato umetokana na kutopata gawio kutoka kwenye benki ya NBC ambapo shirika linasimamia asilimia 30 ya hisa kwa niaba ya Serikali. Aidha, Shirika limesimamia kesi zilizoko mahakamani pamoja na kufuatilia kwa karibu madeni yatokanayo na ubinafsishaji, madeni sugu ya iliyokua Benki ya Taifa ya Biashara, shughuli za ufilisi wa mashirika ya umma na riba kutoka katika benki.

 Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2012/13, shirika linatarajia kukusanya mapato ya jumla ya Shilingi bilioni 12.77 kutoka katika vyanzo mbalimbali ikiwa ni pamoja na : uuzaji wa viwanja na majengo, ukusanyaji wa madeni chechefu, ukusanyaji wa madeni yanayotokana na ubinafsishaji, ufilisi wa makampuni na mapato yanayotokana na riba itakayotolewa na benki kwa amana zake.

HUDUMA ZA BIMA
Mamlaka ya Usimamizi wa Shughuli za Bima – TIRA
Mheshimiwa Spika, sekta ya Bima imeendelea kukua ambapo idadi ya makampuni, madalali na mawakala wa Bima imeongezeka kwa wastani wa asilimia 25.  Mapato kutokana na ada ya bima yameongezeka kutoka shilingi bilioni 286.9 mwaka 2010 hadi shilingi bilioni 342.1 mwaka 2011 sawa na ongezeko la asilimia 19.2. Malipo ya madai ya bima nayo yaliongezeka  kutoka shilingi bilioni 136.4 mwaka 2010 hadi shilingi bilioni 137.4 mwaka 2011. Vitega uchumi vya bima viliongezeka kwa asilimia 16 kutoka shilingi bilioni 254.3 mwaka 2010 hadi shilingi bilioni 296.3 mwaka 2011.  Aidha, Mamlaka imefungua ofisi mbili za kanda katika miji ya Arusha na Mwanza ili kusogeza huduma za usimamizi wa soko karibu na wadau.

Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2012/13, Mamlaka itaandaa Kanuni zitakazosimamia utendaji wa Baraza la Usuluhishi la Bima. Aidha, Mamlaka ya Usimamizi wa Bima itafungua ofisi katika kanda ya nyanda za juu kusini, kwa lengo la kusogeza huduma za usimamizi wa soko karibu na wadau.

Shirika la Bima la Taifa (NIC)

Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2011/12, Wizara iliendelea kulifanyia marekebisho  Shirika la Bima la Taifa ili kuliwezesha kuongeza tija na hatimaye lianze kufanya biashara kwa faida.  Katika kutekeleza malengo yake ya kuhakikisha kuwa madai halali yote ya bima yanalipwa kwa wakati, Shirika limesimamia ulipaji wa malimbikizo ya madai ya muda mrefu ya wateja wake ambapo jumla ya shilingi bilioni 25.32 zimelipwa katika mwaka wa 2011. Kati ya fedha hizo kiasi cha shilingi bilioni 19.98 zilipatikana kutokana na kuuzwa kwa baadhi ya mali ya Shirika isiyoendana na biashara ya msingi (non-core assets) na shilingi bilioni 5.34 ni kutokana na mapato ya biashara (premiums).

Mheshimiwa Spika, mapato ya Shirika la Taifa la Bima yatokanayo na vitega uchumi yameongezeka kutoka shilingi bilioni 6.0 mwaka 2010 hadi shilingi bilioni 16.47 mwaka 2011 ikiwa ni ongezeko la asilimia 174. Aidha, kwa ujumla, mapato ya shirika kutoka vyanzo mbalimbali yaliongezeka kutoka shilingi bilioni 32.91 mwaka 2010 hadi shilingi bilioni 44.38 mwaka 2011.

Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2012/13, Wizara inalenga kuligawa Shirika katika makampuni mawili kwa mujibu wa Sheria ya Bima ya mwaka 2009 ambapo kampuni moja ni kwa ajili ya bima za maisha (Life company) na kampuni nyingine ni kwa ajili ya bima ya kawaida (Non-life company).

MASOKO YA MITAJI NA DHAMANA
Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana – CMSA

Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2011/12, Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana ilitekeleza yafuatayo:  kuanzisha mchakato wa kurekebisha Sheria ya Masoko ya Mitaji na Dhamana, Sura ya 79 ya Sheria za Tanzania; kuratibu ushiriki wa wageni katika soko la mitaji; kutoa elimu kwa umma kupitia usambazaji wa vipeperushi na machapisho mbalimbali yenye elimu na ujumbe kuhusu soko la mitaji; kuweka taratibu za kuanzisha soko la Hatifungani za Serikali za Mitaa (Municipal Bonds) pamoja na Soko la Bidhaa (Commodity Exchange) nchini na ;  Soko la Kukuza Kampuni za Wajasiriamali; kushiriki katika kuboresha sheria za masoko ya mitaji ya Jumuiya ya Afrika Mashariki na; kukamilisha maandalizi ya utekekezaji wa mapendekezo ya kuboresha biashara ya Hatifungani.

Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2012/13, Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana inatarajia kutekekeza yafuatayo: kuandaa Mpango Mkakati wa Mamlaka; kuendelea kutoa elimu kwa umma hususan kuwafikia wananchi walio vijijini; kuendelea kujenga masoko ya mitaji na dhamana kwa kuongeza bidhaa na washiriki; kuandaa sheria mpya ya masoko ya mitaji na dhamana; kuzindua soko la kampuni za ujasiriamali na soko la Hatifungani za Manispaa na Halmashauri za Serikali za mitaa;  Kuendelea kuboresha biashara ya Hatifungani kwa kushirikiana na wadau wengine; na kuweka mazingira yatakayowezesha uanzishwaji wa Soko la Bidhaa (Commodity Exchange) nchini.

Soko la Hisa la Dar es Salaam – DSE
Mheshimiwa Spika,  katika mwaka wa fedha 2011/12 kampuni tatu ziliorodheshwa kwenye soko la hisa na kufanya soko hilo kufikisha jumla ya kampuni 18.  Kampuni hizo mpya ni National Media Group (NMG), African Barrick Gold (ABG) na Precion Air Services Ltd (PAL).  Aidha, kutokana na ongezeko la kampuni idadi ya wawekezaji iliongezeka kutoka 174,013 mwaka 2010/11 hadi 180,882 mwaka 2011/12.  Fahirisi ya Soko la Hisa iliongezeka kutoka 1,264.49 mwezi Julai 2011 hadi 1,437.84 mwezi Juni 2012, sawa na ongezeko la asilimia 4.  Vile vile, thamani ya soko kwa ujumla (Market capitalization) iliongezeka kutoka shilingi bilioni 5,926.60 Mwezi Julai 2011 hadi shilingi bilioni 12,772.79 Mwezi Juni 2012, sawa na ongezeko la asilimia 116. Ongezeko hili kwa sehemu kubwa limechangiwa na Kampuni ya African Barrick Gold ambayo ilikuwa na thamani ya shilingi bilioni 5,396.73 wakati ikiorodheshwa sokoni.  Kwa upande wa hisa za makampuni, hisa zenye thamani ya shilingi bilioni 44.4 ziliuzwa ikilinganishwa na lengo la kuuza hisa zenye thamani ya shilingi bilioni 54.

Mheshimiwa Spika,  kwa mwaka wa fedha 2012/13 DSE itaanza kutekekeza  Mpango Mkakati wa miaka mitano kwa kufanya yafuatayo: kuanzisha hatifungani za akiba (micro savings bond) ambapo zitauzwa kwa viwango vya chini na kwa kupitia mtandao wa malipo kwa njia ya simu ili   kuwafikia wananchi wengi haswa wa kipato cha chini (hadi vijijini).

Dhamana ya Uwekezaji Tanzania – UTT
Mheshimiwa Spika,  katika mwaka wa fedha 2011/12, Dhamana ya Uwekezaji Tanzania ilitekeleza yafuatayo: kuhamasisha uwekaji wa akiba pamoja na dhana ya uwekezaji kupitia elimu kwa umma; kusimamia utendaji na ufanisi katika Ofisi zake za Kanda ili kuwafikia watanzania wengi; na kuimarisha mafanikio yaliyofikiwa na mifuko minne ya uwekezaji wa pamoja iliyokwisha anzishwa yaani – Mfuko wa Umoja, Mfuko wa Wekeza Maisha, Mfuko wa Watoto na Mfuko wa Jikimu. 

Mheshimiwa Spika,  katika mwaka wa fedha 2012/13 Dhamana ya Uwekezaji Tanzania itatekeleza yafuatayo: kuanzisha Mfuko wa uwekezaji wa pamoja wa Dollar Fund; kuanzisha kitengo cha uibuaji wa miradi na usimamizi wake; kuanzisha kitengo/ dirisha la mikopo (Microfinance division); na; kuhamasisha uelewa juu ya dhana ya uwekezaji kupitia elimu kwa umma kwa njia mbalimbali, na kusimamia utendaji wa ufanisi katika Ofisi zake za Kanda.

TAASISI ZA KITAALAM NA HUDUMA NYINGINEZO
Ofisi ya Taifa ya Takwimu – NBS
Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2011/12, Ofisi ya Taifa ya Takwimu ilitekeleza majukumu yake ya kukusanya, kuchambua, kutunza na kusambaza takwimu zilizohitajika katika sekta mbalimbali nchini. Aidha, zoezi la ukamilishaji wa mapitio ya Takwimu za Pato la Taifa kwa bei ya mwaka 2007 linaendelea. Ofisi hii pia, inaendelea na utafiti wa Mapato na Matumizi ya Kaya Binafsi kwa mwaka 2011 ambayo pamoja na mambo mengine takwimu zake zitatumiwa na Serikali pamoja na wadau wengine ili kujua kiwango cha umasikini wa kipato nchini tangu mwaka 2007.

Sensa ya Watu na Makazi
Mheshimiwa Spika, tarehe 26 Agosti, 2012 ni siku ya sensa ya watu na makazi. Sensa itafanyika nchini kote na ni ya tano tangu kuzaliwa kwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mwaka 1964. Kauli mbiu yake ni “SENSA KWA MAENDELEO, JIANDAE KUHESABIWA”.  Lengo kuu la Sensa  ya mwaka 2012, ni kuchangia katika uboreshaji wa maisha ya watanzania kwa kutoa takwimu sahihi na zinazoendana na wakati kwa ajili ya kutunga sera, kupanga mipango ya maendeleo na kuboresha utoaji wa huduma za jamii ikiwa ni pamoja na ufuatiliaji na kutathmini utekelezaji wa programu na maendeleo ya watu.

Mheshimiwa Spika, Sensa ya mwaka huu ina umuhimu wa kipekee kwa maendeleo ya nchi yetu kwa sababu takwimu zitakazokusanywa zitatumika kufuatilia na kutathmini utekelezaji wa Malengo ya Milenia ya mwaka 2015, Dira ya Taifa ya Maendeleo ya mwaka 2025 kwa Tanzania Bara na mwaka 2020 kwa Tanzania Zanzibar pamoja na MKUKUTA kwa Tanzania Bara na MKUZA kwa Tanzania Zanzibar. Aidha, nitumie fursa hii kuwaomba viongozi wenzangu na wananchi kwa ujumla kushiriki na kuhakikisha kuwa tarehe 26 Agosti, 2012 tunahesabiwa bila kukosa.

Bodi ya Taifa ya Wahasibu na Wakaguzi – NBAA
Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2011/12 Bodi ya Taifa ya Wahasibu na Wakaguzi wa Hesabu imetekeleza yafuatayo: kuendesha semina na kongamano 11 kuhusu  matumizi ya viwango vya kimataifa vya utayarishaji na ukaguzi wa taarifa za Hesabu; kuendelea kujenga uwezo wa NBAA; kuhariri mitaala pamoja na silabi ya taaluma ya uhasibu; kuendesha Programu ya Maendeleo Endelevu ya Kitaaluma ambapo jumla ya semina 11 ziliendeshwa; kusimamia ubora wa ukaguzi wa hesabu (Audit Quality Review Scheme) ambapo hadi Juni, 2012 makampuni 50 kati ya 156 yalikaguliwa katika awamu ya kwanza; na Kufanya usajili wa wahasibu na kutunza takwimu.

Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2012/13, NBAA imejipanga kutekeleza majukumu yake yakiwemo: kuendelea kufanya usajili wa watahiniwa, wanachama na makampuni ya uhasibu na ukaguzi; kufanya ukaguzi na kusimamia ubora wa kazi za ukaguzi;  kutoa miongozo ya viwango vya uhasibu na ukaguzi; na kusimamia mradi wa maboresho ya Bodi ya Wahasibu na Wakaguzi wa Hesabu unaoendelea chini ya mshauri elekezi. Aidha, Bodi itaendelea na jukumu la kuendeleza taaluma ya uhasibu pamoja na awamu ya pili ya ujenzi wa Kituo cha Taaluma ya Uhasibu eneo la Bunju wilayani Kinondoni.

Bodi ya Wataalamu wa Ununuzi na Ugavi – PSPTB
Mheshimiwa Spika, kwa mwaka wa fedha 2011/12, Bodi ya Wataalamu wa Ununuzi na Ugavi (Procurement and Supplies Professionals and Technicians Board) ilitekeleza yafuatayo: kuboresha mazingira ya mafunzo kwa kutengeneza na kuzindua tovuti (www.psptb.go.tz) na kanzi data ya wataalam (Professionals Management Information System - PMIS); kusajili wataalamu 991 wa ngazi mbalimbali; kuendesha mafunzo ya kitaaluma ambapo warsha 18 ziliendeshwa katika mikoa 12. Aidha, Bodi imetahini jumla ya wanafunzi 4,532 ambapo 1,689 sawa na asilimia 37.3 walifaulu. Idadi ikijumuishwa na wale wahitimu wa iliyokuwa Bodi ya Taifa ya Usimamizi wa Vifaa (NBMM) inafanya wahitimu kufikia 19,629 kati ya watahiniwa 65,149.

Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2012/13, Bodi itaendelea kutekeleza yafuatayo: kuendelea kuelimisha umma juu ya Sheria namba 23 ya mwaka 2007 ya Bodi  ya wataalamu wa ununuzi na ugavi na kanuni zake; kuelimisha na kuhamasisha wataalamu wa ununuzi na ugavi wazingatie Sheria ya Ununuzi wa Umma (PPA-2011); kuongeza kiwango cha ufaulu wa wanachama toka kiwango cha sasa cha asilimia 37 hadi kufikia asilimia 45; kutafuta wabia watakaoweza kuipatia Bodi vitendea kazi, na kuboresha mazingira ya kazi; na kufanya upembuzi yakinifu wa ujenzi kwenye kiwanja cha PSPTB kilichopo eneo la Luguruni.

Bodi ya Michezo ya Kubahatisha
Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2011/12, Bodi ya Michezo ya Kubahatisha iliendelea kutekeleza majukumu yafuatayo: kutoa leseni kwa waendeshaji wa michezo ya aina mbalimbali ya kubahatisha nchini; kusimamia taratibu za kisheria na kiufundi na ukaguzi wa mara kwa mara wa uendeshaji wa michezo ya kubahatisha ili kuhakikisha michezo hiyo inaendeshwa kwa mujibu wa sheria; na kukamilisha mapendekezo ya marekebisho ya Sheria ya Michezo ya Kubahatisha Na. 4 ya mwaka 2003 na kanuni zake ili kuruhusu uanzishwaji wa michezo ya “internet casino”. Aidha, Bodi imekusanya kodi inayofikia jumla ya Shilingi bilioni 7.2 ikiwa ni asilimia 97 ya lengo la Shilingi bilioni 7.4, ikiwa ni ongezeko la asilimia 16 ikilinganishwa na Shilingi bilioni 6.2 zilizokusanywa mwaka 2010/11. Hadi kufikia Juni, 2012, mapato ya Bodi yalifikia shilingi bilioni 5.43, ikiwa ni ongezeko la asilimia 42 ikilinganishwa na shilingi bilioni 3.8 zilizokusanywa kwa mwaka 2010/11. Vile vile, Bodi imechangia kiasi cha Shilingi milioni 382.6 katika Mfuko Mkuu wa Serikali, ikiwa ni ongezeko la asilimia 45 ikilinganishwa na mchango wa Shilingi milioni 263.7 kwa mwaka 2010/11.

Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha wa 2012/13, Bodi inatarajia kukusanya kodi ya Shilingi bilioni 13.5 ambayo ni ongezeko la asilimia 88 ikilinganishwa na Shilingi bilioni 7.2 kwa mwaka 2011/12. Ongezeko hili linatokana na ubunifu wa vyanzo vipya vya kodi pamoja na kuongezeka kwa vima vya tozo kwa michezo ya kasino.  Vyanzo vipya vinavyotarajiwa kuchangia kuongezeka kwa kodi ni “internet casino”, sms lotteries na sports betting.

ASASI ZA MAFUNZO
Taasisi ya Uhasibu Arusha – IAA
Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2011/12, Taasisi ya Uhasibu Arusha imetekeleza yafuatayo: kuanzisha Shahada ya Uzamili ya Fedha na Uwekezaji kwa ushirikiano na Chuo Kikuu cha Coventry cha Uingereza; kuandaa mitaala kwa ajili ya Stashahada tatu za ambazo ni Stashahada ya Uzamili katika Benki na Fedha, Stashahada ya Uzamili katika Kompyuta na Stashahada ya Uzamili katika Ugavi na Usambazaji; kuweka Samani katika  jengo jipya la maktaba; kuanzisha Kitengo cha  Utafiti wa Teknolojia; na kukamilisha Mfumo wa Student Academic Register Information System (SARIS) ambao utarahisisha upatikanaji wa taarifa zote za kitaaluma na fedha kwa wanachuo popote walipo kupitia mtandao. Aidha, Idadi ya wanachuo imeongezeka kutoka wanachuo 3,394 kwa mwaka 2010/11  na kufikia 3,427 mwaka 2011/12.

Mheshimiwa Spika, kwa ushirikiano na Taasisi ya Teknolojia ya Birla kutoka India, Chuo kinatarajia kuanzisha Shahada tatu za Uzamili ambazo ni Shahada ya Uzamili katika Uhandisi wa Mifumo ya Kompyuta, Shahada ya Uzamili katika Matumizi ya Kompyuta na Shahada ya Uzamili katika Usalama wa Mifumo ya Kompyuta. Kwa sasa mitaala ya shahada hizo inahakikiwa na NACTE. Aidha, udahili wa wanafunzi katika stashahada tatu za uzamili ambazo mitaala yake imeshapitishwa na NACTE unatarajiwa kuanza katika mwaka wa masomo unaoanza Octoba 2012. Vile vile, Chuo kina mpango wa kuanzisha kituo cha elimu kwa masafa (E-Learning Centre). Idadi ya wanafunzi kwa mwaka 2012/13 inatarajiwa kufikia 3,500.

Taasisi ya Uhasibu Tanzania – TIA
Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2011/12, Taasisi iliendelea kuendesha kozi zake kuanzia ngazi ya Cheti, Diploma na Shahada katika fani za Uhasibu, Ununuzi na Ugavi, Rasilimali Watu na Uongozi wa Biashara. Katika kukidhi matakwa ya wadau wake, Taasisi imeendelea na mipango ya kuanzisha kozi ya Uhasibu wa Serikalini (Public Sector Accounting) na tayari zoezi la kuandaa mitaala limekamilika.  Kuanzishwa kwa kozi hii kutatoa mchango mkubwa katika kutoa wahasibu wenye sifa za kufanya kazi serikalini.

 Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2012/13, Taasisi ya Uhasibu Tanzania imepanga kufungua tawi jipya katika Jiji la Mwanza. Kozi zitakazoendeshwa katika tawi hili ni katika fani za Uhasibu, Ununuzi na Ugavi, Rasilimali watu na Uongozi wa Biashara kwa  ngazi ya cheti. Jumla ya wanachuo 600 wanatazamiwa kudahiliwa katika tawi hili. Aidha, Idadi ya wanachuo inatarajia kuongezeka kufikia 8,000 kutoka 6,500 ya mwaka 2011/12.

Chuo cha Usimamizi wa Fedha – IFM
Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2011/12, chuo kimelipa fidia kwa wanavijiji wa Msata na Kihangaiko Wilaya ya Bagamoyo kwa ajili ya kumiliki eneo la ekari 1,500 ambalo litatumika kuanzisha kampasi ya pili itakayoweza kudahili zaidi ya wanafunzi 15,000.

Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2012/13, chuo kinatarajia kutekeleza yafuatayo: kuanzisha shahada mpya za uzamili; kuanzisha kituo cha ufundishaji huko Mwanza; kuongeza na kuboresha mbinu za kukitangaza chuo na kuainisha maeneo ya utafiti na huduma kwa jamii ambayo chuo kinaweza kushirikiana na taasisi zingine.

Chuo cha Mipango na Maendeleo Vijijini – IRDP
Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2011/12, Chuo kimetekeleza yafuatayo; kutoa mafunzo ya muda mrefu katika program kumi za ngazi za Cheti, Stashahada, Shahada na Stashahada za Uzamili kwa wanafunzi wapatao 4,000; kuanzisha mafunzo ya cheti katika kituo cha Mwanza kwa Wanafunzi 320; kujenga uwezo wa watumishi 166 na kuajiri watumishi wapya 14; kukamilisha maandalizi ya Taarifa za Kiuchumi na Kijamii kwa Wilaya za Kondoa, Kilosa na Gairo. Aidha, Chuo kimekamilisha maandalizi ya programu mbili   za Shahada ya Uzamili katika Uchumi na Mipango ya Mazingira.

Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2012/13, Chuo kitatoa mafunzo ya muda mrefu kwa kozi 12 katika ngazi ya Cheti, Stashahada, Shahada, Stashahada ya Uzamili na Shahada ya Uzamili. Aidha Chuo kitaanzisha kozi tatu mpya katika ngazi ya Shahada ya Uchumi wa Maendeleo, Mipango ya Rasilimali Watu na Mipango Miji na Usimamizi wa Mazingira na kuendelea kutoa mafunzo ya programu ya Cheti na Stashahada katika kituo cha Mwanza. Vile vile, Chuo kitaendelea kukamilisha ujenzi wa jengo la pili la Taaluma, kuendelea kujenga uwezo wa watumishi wake na kuajiri watumishi wapya ili kuimarisha ubora wa mafunzo. 

Chuo cha Takwimu Mashariki mwa Afrika – EASTC
Mheshimiwa Spika, Chuo cha Takwimu Mashariki mwa Afrika, kiliendelea kutoa mafunzo ya muda mrefu ya Stashahada na Cheti cha takwimu kwa nchi zinazotumia huduma ya Chuo kwa mwaka 2011/12. Wanafunzi 142 walisajiliwa kati ya hao 83 walisajiliwa kwa kozi ya cheti na 59 kwa Stashahada ya Takwimu ambapo wanawake ni asilimia 30 ya wanafunzi waliosajiliwa. Nchi zilizoleta wanafunzi na uwiano wa wanafunzi wote waliosajiliwa ni Afrika Kusini asilimia 23, Uganda asilimia 4, Zambia asilimia 5, Zimbabwe asilimia 3, Namibia asilimia 1 na Tanzania asilimia 64. Aidha, Chuo kilianza maandalizi ya mtaala wa kutoa mafunzo ya awali (Foundation Course) kwa wanafunzi walioshindwa kupata alama za kutosha kuendelea na kidato tano na cha sita ili waweze kuendelea na masomo ya juu.

Mheshimiwa Spika, Chuo kikiwa ni kituo cha kanda cha Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) katika kuhamasisha matumizi ya takwimu, kilitoa mafunzo yanayohusu uandaaji wa hesabu za mapato na matumizi ya Pato la Taifa kwa baadhi ya nchi za SADC. Mafunzo hayo yalilenga kujenga uwezo wa nchi hizo katika kuchambua vyanzo vya mapato kwa ajili ya kujumuishwa kwenye maandalizi ya hesabu za mapato na matumizi ya nchi hizo na kuwa na ulinganifu wa utendaji katika uandaaji wa Pato la Taifa.  Nchi zilizonufaika na mafunzo hayo ni Tanzania, Afrika Kusini, Botswana, Malawi, Mauritius, Lesotho, Swaziland, Zimbabwe, Angola na Msumbiji.

Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2012/13, Chuo kitaongeza idadi ya kozi zinazotolewa kutoka mbili kufikia tano ambapo moja ya kozi hizo itafanywa kwa ushirikiano na Chuo cha takwimu cha Abidjan, Ivory Coast-ENSEA. Chuo kitaanza kutoa mafunzo kwa njia ya mtandao ili kuwezesha wahitaji wengi kusoma kwa gharama nafuu. Aidha, Chuo kitaendelea na kutekekeza Mpango Mkakati wake ikiwa ni pamoja na kuendelea kuimarisha rasilimali watu ili iendane na mahitaji ya ukuaji wa Chuo. Vile vile, Chuo kitaendelea na maandalizi ya mtaala wa Shahada ya Takwimu itakayoanza mwezi Oktoba, 2012. Sambamba na hilo, Mafunzo ya awali (Foundation Course) yataanza.

Changamoto na Hatua Zilizochukuliwa katika Utekelezaji wa Majukumu ya Wizara  kwa Mwaka wa Fedha 2011/12

Mheshimiwa Spika, pamoja na mafanikio yaliyopatikana, Wizara ilikabiliwa na changamoto mbalimbali. Baadhi ya changamoto ni kama ifuatavyo:

Sheria ya Fedha ya Serikali za Mitaa namba 9 ya mwaka 1982 (Local Government Finances Act No. 9 of 1982) haijaoanishwa na Sheria ya Fedha za Umma SURA 348;
Kudhibiti matumizi ya fedha za umma sambamba na kuongeza mapato ya Serikali;
Kuhuisha  muundo wa utumishi wa kada ya Ukaguzi wa ndani Serikalini ili ujumuishe taaluma nyingine mbali ya uhasibu;
Kuzingatia  kanuni na taratibu zilizoainishwa kwenye Mkakati wa Pamoja wa Misaada Tanzania (MPAMITA);
Kupunguza na kudhibiti mfumuko wa bei ambao umeongezeka kutoka asilimia 13 mwezi Julai 2011 hadi asilimia  17.4 mwezi Juni, 2012;
Kuwianisha uandaaji wa hesabu za majumuisho kutokana na Serikali Kuu kuandaa hesabu zake kwa utaratibu wa “IPSAs Cash Basis” wakati hesabu za Serikali za Mitaa  zinaandaliwa kwa “IPSAs Accrual Basis”;
Kuzingatiwa kwa Sheria ya Ununuzi wa Umma;
Kuwa na watumishi wa kutosha na wenye weledi wa Ununuzi wa Umma na Ukaguzi wa Ndani;
Kupunguza hoja za ukaguzi;
Kuondoa migongano ya sheria ya Msajili wa Hazina na Mashirika anayoyasimamia; na
Kuwa na Sera ya Mali ya Serikali.

Mheshimiwa Spika, katika kukabiliana na changamoto nilizozitaja, hatua zifuatazo zimechukuliwa:-

Kuoanisha Sheria ya Fedha ya Serikali Kuu na Sheria ya Fedha ya Serikali za Mitaa ili kuondoa ukinzani uliopo;
Kuendelea kuimarisha mifumo ya ukusanyaji na usimamiaji wa  mapato yasiyo ya kodi, hususan maduhuli ya Serikali (retention), ikiwa ni pamoja na kuboresha mfumo wa  ukusanyaji kodi ya majengo; 
Kuendelea kufanya mapitio ya sheria mbalimbali zinazotoa misamaha ya kodi;
Kushirikiana na Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma kuendeleza juhudi za kuhuisha kada ya ukaguzi wa ndani;
Kuendelea kuimarisha mfumo wa majadiliano kati ya Serikali na Washirika wa Maendeleo katika ngazi zote kama ulivyoainishwa kwenye MPAMITA;
Kutekeleza awamu ya nne ya Programu ya Maboresho ya Usimamizi wa Fedha za Umma;
Kuendelea kujenga uwezo wa uandaaji, utekelezaji na usimamizi wa bajeti katika ngazi zote za Serikali;
Kuendelea kusimamia udhibiti wa mfumuko wa bei;
Kuendelea kuimarisha mfumo wa malipo kwa njia ya elektroniki na kutoa mafunzo kwa watumiaji;
Kufanya mafunzo  ili kuwezesha uaandaaji wa hesabu kwa kutumia  utaratibu wa “IPSAS Accrual Basis”;
Kuimarisha vitengo vya Ukaguzi wa Awali (Pre – Audit) na Ukaguzi wa Ndani kwa kuviongezea maafisa wenye ujuzi na sifa;
Kukamilisha mchakato wa kuandaa sheria ya Msajili wa Hazina; na
Kuandaa Sera ya Mali ya Serikali.

MAPATO NA MATUMIZI YA  MAFUNGU YA WIZARA KWA MWAKA 2011/12

Fungu 50 – Wizara ya Fedha
Mapato:
Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2011/12, Wizara ilipanga kupata mapato ya Shilingi  bilioni 206.48 kutoka vyanzo mbalimbali vya mapato  yasiyo ya kodi kupitia Fungu hili. Hadi  kufikia Juni, 2012, Fungu 50 lilikusanya mapato yasiyo ya kodi kiasi cha shilingi bilioni 214.62 sawa na asilimia 103.9 ya lengo. Kuvukwa kwa lengo kumetokana na kupata gawio kutoka Benki Kuu ambalo ni kubwa kuliko matarajio pamoja na baadhi ya taasisi ambazo hazikuwa zikichangia kuweza kuchangia kutokana na kuhamasishwa.



Matumizi ya Kawaida:
Mheshimiwa Spika, makadirio ya matumizi ya kawaida kwa mwaka 2011/12 yalikuwa  shilingi bilioni 113.67, kati ya hizo shilingi bilioni 4.32 ni kwa ajili ya mishahara na shilingi bilioni 109.35 ni kwa ajili ya matumizi mengineyo. Hadi kufikia Juni, 2012, matumizi ya kawaida yalifikia shilingi bilioni 102.17. Kati ya matumizi hayo, shilingi bilioni 4.09 yalikuwa ni matumizi ya mishahara na shilingi bilioni 98.08 yalikuwa ni matumizi mengineyo.

Matumizi ya Bajeti ya Maendeleo:
Mheshimiwa Spika, makadirio ya matumizi ya bajeti ya maendeleo yalikuwa jumla ya shilingi bilioni 659.0. Kati ya fedha hizo shilingi bilioni 588 ni kwa ajili ya miradi ya Millenium Challenge Account  Tanzania ikiwemo miradi ya Ujenzi wa Miundombinu ya Usafirishaji, Nishati na Maji. Hadi kufikia Juni, 2012, matumizi yalikuwa shilingi bilioni 402.71, kati ya hizo fedha za ndani ni shilingi bilioni 78.65 na fedha za nje ni shilingi bilioni 324.06.

Fungu 21 – HAZINA
Mapato:
Mheshimiwa Spika, mapato yanayokusanywa na Fungu hili yalifikia shilingi bilioni 6,511.2, sawa na asilimia 104.5 ya lengo la mwaka la kukusanya shilingi bilioni 6,228.8.

Matumizi ya Kawaida:
Mheshimiwa Spika, kwa mwaka 2011/12, bajeti ya Fungu 21 kwa ajili ya matumizi ya kawaida ilikuwa shilingi bilioni 1,003.07. Kati ya fedha hizo mishahara ni shilingi bilioni 1.79 na matumizi mengineyo shilingi bilioni 1,001.28, ambapo, shilingi bilioni 162.41 ni matumizi ya idara na taasisi zilizo chini ya fungu hili, shilingi bilioni 394.88 ni nyongeza ya mishahara ya watumishi wa Serikali, shilingi bilioni 129.76 ni dharura na michango ya kisheria ya mwajiri, na shilingi bilioni 314.24 ni matumizi maalum. Hadi kufikia Juni, 2012 matumizi ya kawaida yalikuwa ni shilingi bilioni 1,002.73, kati ya hizo shilingi bilioni 175.00 ni kwa ajili ya mishahara na matumizi mengineyo ya idara na taasisi zilizo chini ya fungu hili na shilingi bilioni 827.73 ni kwa ajili ya nyongeza ya mishahara ya watumishi wa Serikali,  matumizi maalum na dharura.


Matumizi ya Bajeti ya Maendeleo:
Mheshimiwa Spika,  katika mwaka wa fedha 2011/12, bajeti ya Fungu 21 kwa ajili ya matumizi ya maendeleo ilikua shilingi bilioni 51.49.  Hadi  kufikia Juni, 2012 matumizi ya fedha za maendeleo yalifikia shilingi bilioni 43.50.  Kati ya fedha hizo, shilingi bilioni 24.04 ni fedha za  ndani na shilingi bilioni 19.46 ni fedha za nje.

Fungu 22 – Deni la Taifa
Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2011/12,  bajeti ya Fungu hili ilikuwa shilingi bilioni 2,526.08. Kati ya fedha hizo, malipo ya deni la ndani ni Shilingi bilioni 1,680.99, malipo ya deni la nje ni Shilingi bilioni 171.69 na CFS Others ni Shilingi bilioni 673.40. Hadi kufikia Juni, 2012  matumizi ya Fungu hili yalifikia shilingi bilioni 2,525.91.

Fungu 23 – Mhasibu Mkuu wa Serikali
Matumizi ya Kawaida:
Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2011/12, bajeti ya matumizi ya kawaida kwa Fungu hili ilikuwa shillingi bilioni 82.97, kati ya fedha hizo, mishahara ni shilingi bilioni 3.27 na shilingi bilioni 79.71 ni kwa ajili ya matumizi mengineyo. Hadi kufikia Juni, 2012 matumizi ya kawaida yalikuwa shilingi bilioni 73.75.

Matumizi ya Bajeti ya Maendeleo:
Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2011/12, bajeti ya maendeleo ilikuwa shilingi bilioni 6.86 na matumizi ya maendeleo yalikuwa shilingi bilioni 6.64, kati ya hizo, fedha za ndani ni shilingi bilioni 4.19 na fedha za nje ni shilingi bilioni 2.45.

Fungu 45 – Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi
Matumizi ya Kawaida:
Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2011/12, bajeti ya Fungu hili kwa matumizi ya kawaida ilikuwa shilingi bilioni 34.75. Hadi kufikia Juni, 2012 matumizi ya kawaida yalifikia shilingi bilioni 34.54.

Matumizi ya Bajeti ya Maendeleo:
Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2011/12, bajeti ya maendeleo kwa Fungu hili ilikuwa shilingi bilioni 13.41 kati ya hizo fedha za ndani ni shilingi bilioni 7.55 na fedha za nje ni shilingi bilioni 5.85. Hadi kufikia Juni,2012 matumizi ya maendeleo yalifikia shilingi bilioni 3.89 kwa fedha za nje na shilingi bilioni 4.19 fedha za ndani.

MAKADIRIO YA MAPATO NA  MATUMIZI KWA MWAKA 2012/13
Mapato:
Fungu 50:   Wizara ya Fedha        

Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2012/13, Wizara kupitia Fungu 50  inakadiria kukusanya mapato yasiyo ya kodi yapatayo shilingi  124,420,645,627 (bilioni 124.42)

Fungu 21 - HAZINA:
Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2012/13, Wizara kupitia Fungu 21  inakadiria kukusanya mapato ya kodi yapatayo shilingi  8,070,088,000,000 (bilioni 8,070.09)

MAOMBI YA FEDHA:
Fungu 50:   Wizara ya Fedha        
Mheshimiwa Spika, katika fungu hili kwa mwaka 2012/13, Wizara inaomba kuidhinishiwa kiasi cha fedha kama ifuatavyo:
 (a)         Matumizi ya kawaida shilingi 98,412,912,000 (bilioni 98.41). Kati ya hizo Mishahara ni shilingi 5,852,488,000 (bilioni 5.85) na matumizi mengineyo shilingi 92,560,424,000 (bilioni 92.56).

 (b)         Miradi ya Maendeleo shilingi 546,514,113,000 (bilioni 546.51). Kati ya hizo:
Fedha za Ndani - shilingi 105,532,000,000 (bilioni 105.53).
Fedha za Nje - shilingi 440,982,113,000 (bilioni 440.98).

Fungu 21 - HAZINA:

Mheshimiwa Spika, katika fungu hili kwa mwaka 2012/13, Wizara inaomba kuidhinishiwa kiasi cha fedha kama ifuatavyo:

Matumizi ya kawaida shilingi 725,574,648,000 (bilioni 725.57). Kati ya hizo mishahara ni shilingi 2,508,628,000 (bilioni 2.51) na matumizi mengineyo shilingi 723,066,020,000 (bilioni 723.07) ambazo ni kwa ajili ya matumizi ya Idara na Taasisi zilizo chini ya Fungu hili, nyongeza ya mishahara ya Watumishi wa Serikali, pamoja na matumizi maalum.

(b)          Miradi ya maendeleo ni shilingi 101,955,582,000 (bilioni    101.95) Kati ya hizo;
Fedha za Ndani- shilingi 82,680,039,000 (bilioni 82.68)
Fedha za Nje       - shilingi 19,275,543,000 (bilioni 19.27)

Fungu 22- Deni la Taifa:

Mheshimiwa Spika, katika fungu hili kwa mwaka 2012/13, Wizara inaomba kuidhinishiwa kiasi cha shilingi 2,735,909,673,000 (bilioni 2,735.91). Kati ya hizo deni la nje ni shilingi 373,255,893,000 (bilioni 373.26), deni la ndani ni shilingi 1,583,275,874,000 (bilioni 1,583.27) ikijumuisha kiasi cha shilingi 1,148,106,884,000 (bilioni 1,148.11) kwa ajili ya kulipia hatifungani zinazoiva (Roll-over) na CFS Others shilingi 779,377,906,000 (bilioni 779.38).

Fungu 23 – Mhasibu Mkuu wa Serikali:
Mheshimiwa Spika, katika fungu hili kwa mwaka 2012/13, Wizara inaomba kuidhinishiwa kiasi cha fedha kama ifuatavyo:
Matumizi ya kawaida - shilingi 75,128,765,000  (bilioni 75.13). Kati ya hizo Mishahara shilingi 4,731,503,000  (bilioni 4.73) na matumizi mengineyo shilingi 70,397,262,000 (bilioni 70.39).

 Miradi ya Maendeleo – shilingi 6,122,840,000 (bilioni
        6.12) Kati ya hizo:
(i)           Fedha za ndani -Shilingi 3,500,000,000 (bilioni 3.50).
(ii)          Fedha za Nje  -Shilingi 2,622,840,000 (bilioni 2.62).

Fungu 10 – Tume ya Pamoja ya Fedha:

Mheshimiwa Spika, katika fungu hili kwa mwaka 2012/13, Wizara inaomba kuidhinishiwa kiasi cha shilingi 1,998,246,200 (bilioni 1.99) kwa matumizi ya kawaida. Kati ya fedha hizo shilingi 296,593,000 (bilioni 0.29) ni kwa ajili ya mishahara na matumizi mengineyo shilingi 1,701,653,000 (bilioni 1.70).

 Fungu 13 – Kitengo cha Udhibiti wa Fedha Haramu na Ufadhili wa Ugaidi:

Mheshimiwa Spika, katika fungu hili kwa mwaka 2012/13, Wizara inaomba kuidhinishiwa kiasi cha fedha kama ifuatavyo:
(a)          Matumizi ya kawaida - shilingi 2,163,807,000  (bilioni         2.16) Kati ya fedha hizo Mishahara shilingi 219,017,000         (bilioni 0.22 )      na matumizi mengineyo shilingi    1,944,790,000 (bilioni 1.94).
(b)          Miradi ya Maendeleo, fedha za nje Shilingi 267,800,000 (bilioni 0.27).
              
Fungu 45: Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi

Mheshimiwa Spika, katika fungu hili kwa mwaka 2012/13, Wizara inaomba kuidhinishiwa kiasi cha fedha kama ifuatavyo:
(a)          Matumizi ya kawaida shilingi 55,018,106,000             (bilioni 55.02). Kati ya hizo mishahara ni shilingi  7,980,773,000 (bilioni 7.98) na matumizi mengineyo shilingi 47,038,333,000 (bilioni 47.04).

(b) Miradi ya maendeleo shilingi 9,623,927,000 (bilioni 9.62), kati ya hizo:

Fedha za ndani shilingi 7,500,000,000 (bilioni 7.50).

Fedha za nje shilingi  2,123,927,000 (bilioni 2.12).

Mheshimiwa Spika, napenda kuwashukuru Waheshimiwa Wabunge wote kwa kunisikiliza.

  Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hoja.
Posted by MROKI On Wednesday, August 15, 2012 No comments

0 comments:

Post a Comment

  • Facebook
  • Twitter
  • Youtube

Labels

Blog Archive

Nafasi Ya Matangazo